WHO: Mlipuko wa polio Madagascar umekwisha
(last modified Tue, 20 May 2025 11:59:37 GMT )
May 20, 2025 11:59 UTC
  • WHO: Mlipuko wa polio Madagascar umekwisha

Mlipuko wa ugonjwa wa polio aina ya kwanza au (Type 1) nchini Madagascar umetangazwa kuwa umemalizika. Hii ni kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa leo Jumanne na Shirika la Afya Duniani (WHO).

WHO imesema katika taarifa yake kwamba kesi mpya za polio ziliripotiwa tangu mwezi Septemba mwaka jana, na hivyo kuashiria "hatua muhimu" katika juhudi za kutokomeza polio nchini Madagascar. 

 Septemba mwaka 2023 mlipuko wa polio uliongezeka ambapo kuripotiwa kesi 287 zikiwemo kesi 45 za watu kupooza viungo kwa papo hapo.

Mialy Rajoelina, mke wa Rais wa Madagascar ambaye pia ni balozi wa zoezi la utoaji chanjo ya polio nchini humo, ameeleza kuwa mchakato ulioanzishwa miaka ya karibuni katika kutoa chanjo na kutokomeza polio ni ishara yenye kutia matumaini. 

Ametoa wito wa kuendelea kuchukuliwa hatua za kuzidisha uelewa katika jamii na kushirikiana ili kuwaandalia watoto mustakbali wenye afya.  

Mlipuko huo ulioanza mwaka 2020 na kusababisha hatari kubwa ya kiafya kwa watoto chini ya umri wa miaka mitano na watu wazima ambao hawajachanjwa, ulienea katika wilaya 30 katika mikoa 13 katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki. 

Polio ni ugonjwa wa virusi vya kuambukiza ambao huenea kwa kugusa kinyesi kilichoambukizwa au chakula na maji yaliyochafuliwa. Virusi hivyo vinaweza kuvamia mfumo wa neva na kusababisha viungo vya mwili kupooza.