Sudan: Imarati ilipanga njama za kumuua Abdel Fattah al-Burhan
(last modified Sat, 24 May 2025 02:33:00 GMT )
May 24, 2025 02:33 UTC
  • Sudan: Imarati ilipanga njama za kumuua Abdel Fattah al-Burhan

Sudan imeutuhumu Umoja wa Falme za Kiarabu (UAE) kwa kujaribu kumuua mkuu wa Baraza la Mpito Abdel Fattah al-Burhan, huko Port Sudan.

Mwakilishi wa Kudumu wa Sudan katika Umoja wa Mataifa, al-Harith Idriss al-Harith amesema katika kikao cha dharura cha Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kwamba nchi ya Imarati imetumia hali ya mauaji ili kuiingiza nchi kwenye handaki la giza, kwa sababu nia ni kuchora upya ramani ya Sudan, kusambaratisha vikosi vya jeshi, na kuwaondoa watu wake," akisisitiza kushindwa kwa mpango huo.

Idris alithibitisha, kwa mujibu wa kile kilichoripotiwa na tovuti ya Al-Sudani, kwamba "shambulio la ndege zisizo na rubani za UAE kwenye Bandari ya Sudan tarehe 6 Mei halikulenga tu uharibifu wa maghala ya mafuta, lakini pia lilirusha kombora la usahihi wa hali ya juu katika makao makuu ya Rais Burhan karibu na Hoteli ya Coral, na kusababisha uharibifu mkubwa."

Itakumbukwa kuwa, hivi karibuni serikali ya Sudan ilitangaza kwamba imeamua kuvunja uhusiano wa kidiplomasia na Muungano wa Falme za Kiarabu (Imarati) na kumrejesha nyumbani balozi wake, ikitangaza kuwa Imarati ni "nchi chokozi."

Waziri wa Ulinzi wa Sudan, Yassin Ibrahim Yassin, alisema hayo kwa njia ya televisheni ya serikali na kuishutumu Abu Dhabi kwa kutoheshimu haki ya kujitawala ardhi ya Sudan kupitia kushirikiana kwake na Vikosi vya Msaada wa Haraka RSF vinavyopigana na Jeshi la Sudan SAF kwa muda mrefu sasa.

Mgogoro kati ya jeshi la Sudan SAF na Vikosi vya Msaada wa Harakati RSF umepelekea kuzuka mzozo mbaya zaidi wa kibinadamu duniani na ambao unazidi kuwa mbaya kutokana na mashambulizi kama hayo dhidi ya mji wa Port Sudan. Mji huo una ofisi kuu za Umoja wa Mataifa na mashirika ya misaada, pamoja na wizara za serikali zinazoshikamana na jeshi.