Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila awasili Goma
(last modified Tue, 27 May 2025 02:55:42 GMT )
May 27, 2025 02:55 UTC
  • Rais wa zamani wa DRC Joseph Kabila awasili Goma

Joseph Kabila Rais wa zamani wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amewasili katika mji wa Goma wa mashariki mwa nchi hiyo licha ya kutuhumiwa kushirikiana na makundi ya waasi.

Kiongozi wa muungano wa kisiasa na kijeshi wa waasi wa AFC/M23 Corneille Nangaa, ametangaza kuwa Joseph Kabila amewasili jana katika mji wanaoudhibiti wa Goma.

Corneille Nangaa amesema kwa pamoja na Kabila wamedhamiria kukomesha kile alichokiita udikteta na migawanyiko nchini Jamhuri ya Kidemokrasia yay Congo.

Kurejea kwa Kabila nchini Kongo kumethibitishwa pia na watu wa karibu yake. Kikaya Bin Karubi aliyekuwa mshauri wake wa masuala ya kisiasa na kidiplomasia ameziambia duru za habari kwamba Kabila aliwasili usiku wa kuamkia jana, lakini hakueleza ajenda na muda ambao kiongozi huyo wa zamani wa Kongo atasalia katika mji huo.

Duru nyingine ya karibu na Joseph Kabila imesema ziara hiyo ni yamshikamano na raia wa Kivu walioathirika na vita na kwamba ana mpango wa kurejesha amani ambao atawawakilisha pia kwa waasi wa AFC/M23.

Kabila anafanya ziara hiyo siku chache baada ya Bunge la Seneti la nchi hiyo kumuondolea kinga ya kutoshtakiwa, na kufungua njia ya mwanasiasa huyo kufunguliwa mashtaka.

Kabila anatuhumiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita, na kuunga mkono kundi la waasi la M23 ambalo liliteka miji mikubwa Mashariki mwa Congo mapema mwaka huu.

Joseph Kabila anakuwa mkuu wa kwanza wa zamani wa nchi huko DRC kushtakiwa kwa uhaini, uhalifu wa kivita na mashtaka yanayohusiana nayo. Uamuzi huo  wa Bunge la Seneti sasa unatoa nafasi kwa mahakama ya kijeshi kuanzisha kesi dhidi yake.