Aliyenajisi mabinti 100 Malawi kufungwa jela maisha?
Mahakama moja nchini Malawi imemnyima dhamana mwathirika wa virusi vya HIV aliyewanajisi mabinti wadogo zaidi 100 kwa madai ya kuwasafisha na kuwafanyia tambiko la kimila na kiutamaduni.
Hakimu Anderson Masanjal amesema mahakama hiyo imeafiki kumrejesha rumande Eric Aniva mwenye umri wa miaka 45 ili uchunguzi wa madai ya ubakaji dhidi yake ukamilike. Iwapo atapatikana na hatia, mshukiwa huyo anaweza kuhukumiwa kifungo cha maisha jela.
Aniva alikamatwa mwishoni mwa mwezi uliopita wa Julai kufuatia amri ya Rais Peter Mutharika wa nchi hiyo, baada ya kukiri kwamba amefanya ngono na watoto wadogo 104 kwa kulipwa fedha na wazazi wao, ikiwa ni sehemu ya utamaduni wa jamii moja ya kusini mwa nchi hiyo. Eric Aniva wa wilaya ya Nsanje alikiri kwamba amefanya ngono na wasichana wadogo kwa kulipwa fedha ambazo ni sawa na kati ya dola nne na saba za Marekani kwa kumbikiri kila mtoto mmoja.
Ripoti zinasema jamii hiyo ya kusini mwa Malawi imekuwa na utamaduni wa kukabidhi watoto wao wa kike wenye umri wa kati ya miaka 11 na 14 wakati wa hedhi yao ya kwanza, kwa mtu huyo anayejulikana kwa jina la 'fisi ili wabikiriwe wakiwa na imani kwamba, ubikira ni mkosi na kwamba kitendo hicho kinawasafisha watoto hao pamoja na jamii hiyo.
Kesi dhidi ya mtuhumiwa huyo mwenye wake wawili inatazamiwa kuendelea Agosti 15 mwaka huu.