Watu saba wauawa Ethiopia katika maandamano ya kupinga serikali
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i12772-watu_saba_wauawa_ethiopia_katika_maandamano_ya_kupinga_serikali
Duru za kuaminika zimeripoti kuwa watu saba wameuawa nchini Ethiopia katika maandamano ya kupinga serikali.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 06, 2016 23:50 UTC
  • Watu saba wauawa Ethiopia katika maandamano ya kupinga serikali

Duru za kuaminika zimeripoti kuwa watu saba wameuawa nchini Ethiopia katika maandamano ya kupinga serikali.

Kwa mujibu wa duru hizo watu wasiopungua saba wameuawa katika makabiliano yaliyotokea kati ya askari polisi na waandamanaji katika mji wa Nemekte Wollega magharibi mwa nchi hiyo. Duru hizo zimeongeza kuwa kwa miezi kadhaa sasa watu wa makabila mawili ya Oromo na Amhara wamekuwa wakimiminika mabarabarani kuandamana wakilalamikia siasa za serikali ya Addis Ababa.

Waziri Mkuu wa Ethiopia, Hailemariam Desalegn

Makabila hayo mawili yanaituhumu serikali ya Waziri Mkuu Hailemariam Desalegn kuwa inafanya ubaguzi kwa kulipendelea kabila la Tigre. Kabila hilo linatuhumiwa kuwa watu wake ndio walioshika nyadhifa nyingi zaidi serikalini na ndio waliojaa kwenye vikosi vya usalama vya nchi hiyo.

Merera Gudina, Kiongozi wa chama cha Kogresi ya Watu wa Omoro

Dakta Merera Gudina, mmoja wa shakhsia mashuhuri wanaoipinga serikali ya Ethiopia na kiongozi wa chama cha Kongresi ya Watu wa Omoro ameashiria hatua ya serikali ya kukata mitandao ya kijamii na kueleza kwamba hali halisi ya mambo haieleweki na kwamba habari zinazowafikia ni za utata na mawasiliano yamekatwa. Gudina amesisitiza kuwa maandamano ya sasa  ni harakati ya pamoja na uasi wa kiraia inayodhihirisha hasira na ghadhabu za wananchi dhidi ya utawala.../