Eswatini kuwatimua wahamiaji 'sugu' kutoka US baada ya malalamiko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i128422
Serikali ya Eswatini ilisema jana Jumatano kwamba, inawashikilia raia watano wa nchi ya tatu waliofukuzwa kutoka Marekani katika magereza yaliyotengwa, chini ya makubaliano na utawala wa Rais Donald Trump, lakini inapania kuwarejesha katika nchi zao.
(last modified 2025-07-22T07:00:06+00:00 )
Jul 17, 2025 04:59 UTC
  • Eswatini kuwatimua wahamiaji 'sugu' kutoka US baada ya malalamiko

Serikali ya Eswatini ilisema jana Jumatano kwamba, inawashikilia raia watano wa nchi ya tatu waliofukuzwa kutoka Marekani katika magereza yaliyotengwa, chini ya makubaliano na utawala wa Rais Donald Trump, lakini inapania kuwarejesha katika nchi zao.

"Kwa kweli, wafungwa hao watano kwa sasa wamewekwa katika vituo vyetu vya kurekebisha tabia katika magereza yaliyotengwa, ambapo wahalifu sawa na hao wanawekwa," amesema kaimu msemaji wa serikali ya Eswatini, Thabile Mdluli katika taarifa.

Amewahakikishia wananchi wa Eswatini kwamba wafungwa hao si tishio kwa nchi au raia wake na kueleza kuwa, "Serikali inafahamu wasiwasi ulioenea kuhusu kufukuzwa kwa wafungwa wa nchi ya tatu kutoka Marekani hadi Ufalme wa Eswatini."

Taarifa hiyo imekuja baada ya wananchi wa Eswatini hususan vijana katika mitandao ya kijamii kukosoa vikali hatua ya utawala huo wa kifalme kukubali 'kugeuzwa jalala' la kuwapokea wahamiaji sugu ambao wameshawahi kupatikana na hatia ya kufanya uhalifu nchini Marekani.

Idara ya Usalama wa Ndani ya Marekani ilisema Jumanne kwamba, ndege ya kuwahamisha wahamiaji hao kutoka nchi tano ilitua Eswatini, baada ya Mahakama ya Juu ya US kuondoa vikwazo vya kuwapeleka wahamiaji katika nchi ambazo si zao.

Ubalozi wa Marekani nchini Eswatini ulitoa taarifa ambayo ilijaribu kuondoa hofu ya umma kuhusu wafungwa hao. Msemaji wa ubalozi huo, Carly Van Orman alithibitisha kwamba wahamiaji hao wako chini ya ulinzi mkali wa mamlaka ya Eswatini.

Wahajiri hao waliofukuzwa US ni raia wa Cuba, Jamaica, Laos, Vietnam na Yemen. Kwa mujibu wa Idara ya Usalama wa Taifa ya Marekani, wahamiaji hao walipatikana na hatia ya uhalifu wa kutumia mabavu kama ubakaji wa watoto na mauaji.