Mamia waandamana Tunis kuwaunga mkono Wapalestina wanaokabiliwa na njaa Gaza
Mamia ya wananchi wa Tunisia jana Jumatatu walifanya maandamano katika mitaa mbalimbali ya mji mkuu wa nchi hiyo Tunis kuonyesha mshikamano mkubwa na wananchi wa Palestina kutokana na hali mbaya ya kibinadamu inayoendelea Gaza.
Waandamanaji walibeba bendera za Palestina huku wakipiga nara za kukosoa na kulaani mzingiro dhidi ya Gaza na kimya cha nchi za Kiarabu mkabala wa masaibu wanayopitia watu wa eneo hilo.
Lotfi Mloudi raia wa Tunisia aliyeshiriki kwenye maandamano alinukuliwa akisema:" Njaa huko Gaza imefikia pabaya. Wananchi wa Palestina wanaaga dunia kwa kukosa chakula. Wanasababishiwa njaa kwa makusudi na si na Wazayuni pekee yao bali pia baadhi ya mataifa ya Kiarabu yanahusika katika maafa hayo."
Wananchi wa Tunisia waliomiminika katika mitaa mbalimbali ya Tunis wameitaja hatua ya nchi za Kiarabu ya kuanzisha uhusiano wa kawaida na utawala wa Kizayuni kuwa ni usaliti.
"Nchi zote za Kiarabu zinapasa kuchukua hatua zaidi katika uwanja huu. Maandamano ni muhimu kwa ksababu kimya hakisaidii", ameendelea kueleza raia huyo.
Ahmed Nejiv Chebbi mwanasiasa mtajika kwa upinzani wa nchini Tunisia ambaye ni Mkuu wa harakati ya Ukombozi wa Kitaifa ya nchi hiyo ameshiriki bega kwa bega na Watunisia wengine katika maandamano hayo dhidi ya utawala haramu wa Israel.
Juzi Jumapili pia maelfu ya wananchi wa Morocco waliandamana mkabala wa bandari kubwa zaidi ya nchi hiyo huko Tanger Med kaskazini mwa nchi hiyo kupinga kutia nanga meli zilizobeba silaha za utawala ghasibu wa Israel.