RSF yashambulia kambi ya Abu Shouk Darfur Kaskazini
Wanamgambo wa RSF wameishambulia kambi ya wakimbizi wa ndani ya Abu Shouk katika mkoa wa Darfur Kaskazini na kusababisha mauaji ya watu 40 huku wengine 19 wakijeruhiwa vibaya.
Kundi la wanaharakati wa haki za binaadamu wanaotoa msaada kote nchini Sudan, limesema wanamgambo hao wanaopambana na jeshi la Sudan, wanasemekana kushambulia sehemu ya kambi hiyo na kuwalenga raia ndani ya nyumba zao.
Wanaharakati hao wamesema mashambulizi hayo yanadhihirisha kiwango cha kutisha cha ukiukaji unaofanywa na RSF dhidi ya watu wasio na hatia wala ulinzi wowote.
Awali msemaji wa Umoja wa Mataifa, Stephane Dujarric alitahadharisha juu ya hali mbaya inayoendelea kushuhudiwa nchini Sudan.
Jeshi la Sudan na Vikosi vya Usaidizi wa Haraka vimekuwa vikikabiliana katika vita vya umwagaji damu na uharibifu tangu Aprili 2023, ambapo juhudi za upatanishi za kikanda na kimataifa hazijafanikiwa kumaliza vita hivyo hadi sasa.
Hayo yanajiri katika hali ambayo, mashirika ya kieneo na kimataifa yameendelea akutoa indhari kuhusiana na kuzidi kuwa mbaya hali ya kibinadamu nchini Sudan.
Kusimamishwa kwa ufadhili wa kimataifa wa fedha kunakisukuma kizazi chote cha watoto wa Sudan katika ukingo wa madhara yasiyoweza kurekebishwa huku idadi ya watoto walioathiriwa na utapiamlo nchini humo ikiongezeka. Haya ni kwa mujibu wa ripoti ya UNICEF.
Mpango wa Chakula Duniani (WFP) ulisema mwezi Julai mwaka huu kuwa, maeneo kadhaa ya kusini mwa mji mkuu wa Sudan, Khartoum, yako katika hatari ya kukumbwa na njaa.
Wakati huo huo Ofisi ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu ya Umoja wa Mataifa imeripoti kuwa: Ni asilimia 23 tu ya mpango wa kimataifa wa misaada ya kibinadamu wa dola bilioni 4.16 kwa Sudan ambayo imetolewa hadi sasa.