Araqchi: Umewadia wakati wa vikwazo kutambuliwa kama jinai dhidi ya ubinadamu
-
Abbas Araqchi, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran
Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran amesisitiza kuwa: "Wakati umefika kwa vikwazo visivyo vya kibinadamu vilivyowekwa na Marekani na washirika wake kutambuliwa kuwa ni jinai dhidi ya binadamu."
Akizungumzia vikwazo vilivyowekwa na Marekani na nchi za Magharibi, Sayyid Abbas Araqchi ameandika kwenye akaunti yake rasmi kwenye mtandao wa kujamii wa X: Tawala za Magharibi zimekuwa zikidai kwamba vikwazo ni njia mbadala isiyo na damu ya vita. Lakini ukweli ni upi?
Araqchi amesema: "Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida maarufu la The Lancet unaonyesha kuwa, vikwazo vya upande mmoja, hasa vile vilivyowekwa na Marekani, vinaweza kuwa vibaya kama vita vya mauaji." Waziri Araqchi amebainisha kuwa, tangu miaka ya 1970, zaidi ya watu 500,000 wanapoteza maisha kila mwaka kutokana na vikwazo; na waathirika wakuu wamekuwa ni watoto na wazee.

Waziri wa Mashauri ya Kigeni ya Jamhuri ya Kiislamu ya Iran ameeleza kuwa: "Wakati umefika kwa vikwazo hivi visivyo vya kibinadamu, vilivyowekwa na Marekani na washirika wake, kutambuliwa kama uhalifu na jinai dhidi ya ubinadamu." Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran pia ameandika: Nchi zilizowekewa vokwazo lazima zijibu ukandamizaji huu uliopangwa kwa njama zilizoratibiwa, kwa kuwa na umoja kuhusiana na hili.
Marekani na washirikka wake wa Magharibi wamekuwa wakitumia vikwazo kama wenzo wa kukabiliana na mataifa yasiyokubali kufuata sera zao.
Iran, Venezuela na Russia ni miongoni mwa mataifa ambayo katika miaka ya hivi karibuni yameandamwa na vikwazo haramu vya Marekanai na washirika.