Mamia waandamana Barcelona kupinga mauaji ya kimbari ya Israel Gaza
-
Maandamamo ya mamia ya Wahispania mjini Barcelona kupinga vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza.
Mamia ya Wahispania wameandamana mjini Barcelona kupinga vita vya mauaji ya halaiki vya utawala wa Israel dhidi ya Gaza.
Waandamanaji hao wakiwa wamebeba mabango na maberamu na wakipiga nara dhidi ya Israel wamelaani mauaji ya kimbari ya Israel Gaza na vizuizi vya chakula na dawa na kuuawa kwa waandishi wa habari zaidi ya 230 kati yao watano walikuwa waandishi wa Al-Jazeera katika siku za hivi karibuni.
Waandamanaji hao walibeba picha za waandishi wa habari waliouawa katika shambulio la bomu la Israel kwenye hema lao karibu na hospitali ya Gaza, wakiyataja mashambulizi hayo kuwa ni jaribio la Netanyahu kunyamazisha ukweli. Walishikilia mabango yaliyosomeka: "Wale wanaolenga waandishi wa habari wanaogopa ukweli."
Waandamanaji hao pia waligonga vyungu vitupu, kuashiria janga la njaa Gaza, katika maandamano makali dhidi ya sera ya makusudi ya Israel ya njaa kupitia vizuizi vyake na kukataa kuruhusu chakula na misaada ya matibabu kuingia ukanda huo.

Wakazi wa Barcelona walipeperusha bendera za Palestina na kuimba "Palestina Huru" wakitangaza mshikamano na raia wanaodhulumiwa wa Gaza, ambao wamevumilia karibu miaka miwili ya mashambulizi ya Israel, kuzingirwa kikamilifu, na njaa iliyobuniwa.
Katika kukabiliana na siasa za jinai za utawala wa Kizayuni kwa wananchi wa Palestina, kumekuwa kukifanyika maandamano kadhaa makubwa katika miji mbalimbali duniani.
Hivi karibuni mjini New York, Marekani kundi la wanaharakati wa haki za binadamu na haki za kiraia walikusanyika mbele ya ubalozi mdogo wa Israel, wakiwa wameshikilia bendera za Palestina na kupiga nara dhidi ya utwala huo vamizi na ukiukaji wa haki za binadamu, wakitaka kukomeshwa kwa vita na mzingiro dhidi ya Gaza.