Sudan Kusini yakanusha kukubali kuwapokea Wapalestina kutoka Gaza
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i129512
Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan Kusini imekanusha ripoti zinazosema kwamba imefanya mazungumzo na Israel kuhusu suala la kuwapokea Wapalestina kutoka eneo la Gaza lililokumbwa na vita.
(last modified 2025-08-14T09:11:01+00:00 )
Aug 14, 2025 06:40 UTC
  • Wakazi wa Gaza wakilazimika kuyaham makazi yao
    Wakazi wa Gaza wakilazimika kuyaham makazi yao

Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan Kusini imekanusha ripoti zinazosema kwamba imefanya mazungumzo na Israel kuhusu suala la kuwapokea Wapalestina kutoka eneo la Gaza lililokumbwa na vita.

Taarifa ya Wizara ya Mashauri ya Kigeni ya Sudan Kusini imeyataja madai hayo kuwa hayana msingi na hayaakisi msimamo rasmi au sera ya serikali ya Juba.

Hata hivyo, wizara ya mambo ya nje ya Sudan Kusini imekiri kumpokea naibu waziri wa mambo ya nje wa Israel Sharren Haskel, aliyezuru Juba jana na kusema kwamba ziara hiyo ililenga kuimarisha ushirikiano wa nchi hizo mbili.

Awali chombo kimoja cha habari cha lugha ya Kiebrania kilitangaza kuwa, huku mashambulizi na vita katika Ukanda wa Gaza vikiendelea, Israel inafanya mazungumzo na Sudan Kusini, Indonesia, Libya, Ethiopia na nchi nyingine kadhaa za Kiafrika ili kuwapokea wakaazi wa Ukanda wa Gaza.

Itamar Eisner, ripota wa tovuti ya habari ya lugha ya Kiebrania ya Ynet, alifichua katika ripoti yake kuhusu suala hilo kwamba, Israel kwa sasa inafanya mazungumzo na nchi tano, ikiwa ni pamoja na Sudan Kusini ili kuwakubali wakazi wa Gaza ambao watahamishwa kwa nguvu kutoka eneo hilo.

Baadhi ya ripoti zinasema kuwa, mazungumzo yanaendelea na Indonesia, Libya, Ethiopia, na nchi nyingine ya Afrika kuwakubali Wagaza. Ikinukuu ripoti ya shirika la habari la Associated Press, chombo hicho cha habari cha lugha ya Kiebrania kiliesema kuwa, vyanzo sita tofauti vimethibitisha kuwa mazungumzo kati ya Israel na Sudan Kusini yanaendelea, lakini kiwango cha hatua iliyopigwa katika suala hili bado hakijabainika.