Ufaransa yarejesha mafuvu ya vichwa Madagascar miaka 127 baada ya mauaji ya kikoloni
Ufaransa jana Jumanne ilirejesha mafuvu matatu nchini Madagascar, likiwemo moja linaloaminika kuwa la mfalme aliyekatwa kichwa na wanajeshi wa Ufaransa kufuatia mauaji ya Agosti 1897.
Waziri wa Utamaduni wa Ufaransa, Rachida Dati, alisema katika hafla ya kurudisha mabaki hayo nchini Madagascar kwamba: "Mafuvu haya yaliingizwa katika makusanyo ya kitaifa katika mazingira ambayo yalikiuka wazi utu wa binadamu na katika mazingira ya ukatili wa kikoloni."
Mwenzake wa Madagascar, Volamiranty Donna Mara amesema kwamba: "Kutokuwepo kwa mafuvu hayo nchini kumekuwa jeraha wazi katika moyo wa kisiwa chetu kwa zaidi ya karne moja."
Waziri Mara amesema serikali ya Madagascar inapanga kutoa heshima kwa mabaki hayo katika kumbukumbu ya kunyongwa kwa Mfalme Toera mwishoni mwa Agosti 1897, wakati wa ukoloni wa Ufaransa kisiwani humo.
Wanasayansi wamethibitisha kwamba mafuvu hayo ni ya watu wa Sakalava magharibi mwa Madagascar. Wamesema kuna uwezekano mkubwa kwamba moja ya mafuuvu hayo ni la Mfalme Toera, ambaye aliuawa na wakoloni wa Kifaransa katika mji mkuu wake wa kifalme, Dembi, pamoja na mamia kadhaa ya raia wake.
"Haijabainika wazi iwapo aliuawa kwa kupigwa risasi, na kisha kichwa chake kukatwa, au alikufa kwa sababu ya kukatwa kichwa," amesema mwanahistoria Klara Boyer-Rossol na kuongeza kuwa: "Lakini kichwa chake kilitoweka. Na hivyo wajukuu walinyimwa kichwa cha kifalme cha babu yao."
Boyer-Rossol, ambaye ni mtaalamu wa biashara ya utumwa na utumwa katika eneo la magharibi mwa Bahari ya Hindi, amesema rekodi zilizoandikwa zinaelezea kilichotokea kwa kina.
"Tuna nyaraka nyingi sana zilizoandikwa ambazo zinaeleza kwa uwazi kabisa kwamba Mfalme Toera aliweka silaha chini na kujisalimisha na hivyo aliposhambuliwa na askari wa Kamanda Augustin Gérard, hakuwa na silaha, ndiyo maana tunayataja kuwa mauaji," amesema.
Mafuvu hayo yamekuwa katika makumbusho ya Paris tangu 1897.
Wanajeshi wa Ufaransa walimkata kichwa Mfalme Toera wakati wa mauaji ya wenyeji mnamo 1897, na fuvu lake likapelekwa Ufaransa kama kombe la ushindi, na kuwekwa kwenye jumba la kumbukumbu za historia la kitaifa la Paris pamoja na mamia ya mabaki mengine kutoka katika kisiwa hicho cha Bahari ya Hindi.