Waislamu Nigeria wataka kuachiwa huru kiongozi wa Palestina
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imelaani vikali hatua ya polisi ya Nigeria kumkata kiongozi wa Jumuiya ya Wapalestina katika nchi hiyo ya Afrika Magharibi, Ramzy Abu Ibrahim, ikisisitiza kuwa kukamatwa huko kunafungamana na makubaliano ya hivi karibuni ya usalama kati ya Nigeria na utawala wa Israel.
Taarifa ya harakati hiyo imesema, "Tumepokea taarifa za kukamatwa kwa Ramzy Abu Ibrahim, kiongozi wa Jamii ya Wapalestina nchini Nigeria na polisi wa Nigeria. Chanzo cha kuaminika kilithibitisha kwamba, alikamatwa Ijumaa, Agosti 22, 2025, na kukamatwa huko kulifanyika mwezi huu ambapo Serikali ya Nigeria na dola haramu la Israel zilisaini mkataba wa usalama."
Imebainisha kuwa, "Mabadiliko ya ghafla ya 'undumakuwili' na mabadiliko ya sera ya mambo ya nje ya Nigeria kuhusu Palestina yanaashiria kwamba, utawala unaoongozwa na Bola Ahmad Tinubu umeamua kushirikiana na taifa haramu la Israel katika mauaji ya kimbari yanayoendelea Gaza, Palestina."
Taarifa hiyo imesisitiza kuwa: Jambo hili halikubaliki, linapaswa kulaaniwa, na linaweza kuiweka Nigeria na watu wa nchi hii katika upande mbaya wa historia ya dunia, na matokeo yake ni hatari na yasiyoweza kurekebishika.
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria imeeleza bayana kuwa, "Bola Ahmad Tinubu ameamua kusimama na dola haramu la Israel wakati ambapo nchi kama Uingereza, Ufaransa, Canada, Australia na nyingine kadhaa zinazidi kujitenga na taifa hilo haramu na kushinikiza kutambuliwa kwa taifa la Palestina."
Kujifungamanisha kwa Nigeria na utawala wa Kizayuni wa Israel kunakwenda kinyume na ongezeka la kutengwa kimataifa kwa Israel kutokana na uvamizi wa Gaza, huku kesi za mauaji ya halaiki zikiwasilishwa katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki, mbali na utawala huo kusakamwa na vikwazo vya kibiashara vya nchi nyingi. Aidha hatua ya Tinubu kujikurubisha kwa Israel kunapingana na uungaji mkono wa kihistoria wa Nigeria kwa Palestina ulioanza mwaka 1988.
Haya yanajiri wiki moja baada ya shirika la kimataifa la kutetea haki za binadamu la Amnesty International nchini Nigeria kulaani vikali ukandamizaji mkali wa vyombo vya serikali dhidi ya Waislamu wa madhehebu ya Shia, wakati wa maandamano ya kulaani jinai za Israel dhidi ya Wapalestina wa Gaza, na kusema kuwa takriban wanachama 83 wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria bado wako rumande bila kufunguliwa mashtaka, licha ya kupata majeraha ya risasi na makovu mengineo wakishiriki maandamano ya amani.