Nchi za Afrika zalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Doha
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i130722-nchi_za_afrika_zalaani_mashambulizi_ya_israel_dhidi_ya_doha
Nchi kadhaa za Afrika pamoja na Umoja wa Afrika (AU) zimetoa taarifa kali kulaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala wa Israel siku ya Jumanne, yaliyolenga uongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, nchini Qatar, wakionya kuwa kitendo hicho ni uvunjaji wa wazi wa mamlaka ya taifa hilo la Ghuba ya Uajemi.
(last modified 2026-04-29T03:42:39+00:00 )
Sep 12, 2025 22:57 UTC
  • Nchi za Afrika zalaani mashambulizi ya Israel dhidi ya Doha

Nchi kadhaa za Afrika pamoja na Umoja wa Afrika (AU) zimetoa taarifa kali kulaani mashambulizi ya anga yaliyofanywa na utawala wa Israel siku ya Jumanne, yaliyolenga uongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Kupigania Ukombozi wa Palestina, Hamas, nchini Qatar, wakionya kuwa kitendo hicho ni uvunjaji wa wazi wa mamlaka ya taifa hilo la Ghuba ya Uajemi.

Mwenyekiti wa Tume ya Umoja wa Afrika, Mahamoud Ali Youssouf, ameonya kuwa shambulizi hilo linaweza kuzidisha hali tete ya Mashariki ya Kati (Asia Magharibi), akisisitiza umuhimu wa kuhifadhi utulivu wa kikanda. Aidha amekumbusha nafasi ya Qatar kama mpatanishi wa muda mrefu na mjumbe wa amani, akitoa wito wa “mazungumzo mapya kuelekea amani ya haki na ya kudumu katika Mashariki ya Kati.”

Katika taarifa rasmi ya tarehe 11 Septemba, Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya imepinga hujuma hiyo ya Israel dhidi ya Qatar kwa kusema: “Shambulizi hilo la Israel si tu uvunjaji wa mamlaka na uhuru wa ardhi ya Taifa la Qatar, bali pia ni tishio kubwa kwa amani na usalama wa kikanda na kimataifa.” Wizara ya Mambo ya Nje ya Kenya iliongeza kuwa: “Kitendo hiki kinakiuka sheria za kimataifa, kinadhoofisha misingi ya amani na usalama ambayo sote tunapaswa kuilinda, na hakilingani na Azimio la Umoja wa Mataifa la mwaka 1970 kuhusu Mahusiano ya Kirafiki na Ushirikiano kati ya Mataifa.”

Rwanda nayo pia imelaani uchokozi huo wa Israel dhidi ya Qatar na kusema: “Kukanyaga kwa makusudi misingi ya mahusiano ya mataifa (na Israel) ni hatari, na kunaisukuma dunia kuelekea utaratibu usio na kanuni, hali isiyokuwa na mfano wa kisasa.”

Kauli za Kigali na Nairobi zilifuata tamko la awali la Nigeria, iliylaani uchokozi huo wa Israel dhidi ya Qatar kwa kusema: “ kuna umuhimu wa kuheshimu mamlaka ya kila taifa na kufuata sheria za kimataifa, hasa katika masuala yanayohusisha matumizi ya nguvu nje ya mipaka.”

Somalia, kwa upande wake, ilitoa wito kwa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua za haraka kukomesha vitendo vya uchokozi vinavyofanywa na Israel na kuhakikisha ulinzi wa raia.

Wizara ya Mambo ya Nje ya Misri pia ilitaja shambulizi hilo kuwa “uvunjaji wa wazi wa sheria za kimataifa na mamlaka ya kitaifa.” Wizara ya Mambo ya Nje ya Morocco ililaani “uchokozi wa Israel na kuvunjwa kwa mamlaka ya taifa la ndugu Qatar.” Algeria kwa upande wake, kupitia tamko rasmi, ilisema inalaani vikali “uchokozi wa kikatili wa Israel,” sambamba na kutangaza “mshikamano kamili na wa dhati na taifa la dada Qatar katika kipindi hiki kigumu.”

Vyombo vya habari vya Israel viliripoti kuwa ndege za kivita za utawala huo zilirusha makombora 12 katika makao ya viongoziw Hamas jijini Doha. Hamas ilithibitisha kuwa wanachama wake watano waliuawa katika shambulizi hilo, ambalo Qatar imelilaani vikali.

Wito umeongezeka kwa jumuiya ya kimataifa kuchukua hatua dhidi ya Waziri Mkuu wa Israel, Benjamin Netanyahu, ambaye anakabiliwa na hati ya kukamatwa kutoka Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu (ICC).

Kikao cha dharura cha nchi za Kiislamu na Kiarabu kitafanyika mjini Doha siku ya Jumapili na Jumatatu kwa wito wa serikali ya Qatar, ili kuwaunga mkono Wapalestina wa Ghaza na kuchukua hatua dhidi ya shambulio la hivi karibuni lililofanywa na utawala wa kizayuni wa Israel katika mji mkuu wa Qatar, Doha.