Upinzani Sudan Kusini wapuuzilia mbali mashtaka dhidi ya Machar
Mrengo wa upinzani nchini Sudan Kusini umepuuzilia mbali mashtaka dhidi ya kiongozi wao ambaye pia ni makamu wa rais Riek Machar.
Chama hicho kimesema mashtaka hayo yamebuniwa na yananuiwa kuisukuma nchi katika utawala wa kiimla.
Siku ya Alkhamisi Riek Machar, Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan Kusini alifunguliwa mashitaka ya mauaji, uhaini na uhalifu dhidi ya binadamu.
Mashtaka hayo yanatokana na madai ya kuhusika kwake katika mashambulizi ya wanamgambo dhidi ya vikosi vya serikali mwezi Machi, Waziri wa Sheria amesema hayo juzi Alkhamisi.
Serikali ya Sudan Kusini inadai kuwa, Jeshi Jeupe (White Army), kundi la vijana wanaobeba silaha, lilishambulia kambi ya kijeshi huko Nasir, kaskazini mashariki mwa Sudan Kusini, na kuua zaidi ya wanajeshi 250 kwa amri ya Machar.
Makubaliano tete ya kuwa na serikali ya pamoja kati ya rais Salva Kiir na mpinzani wake wa muda mrefu Riek Machar, yamekuwa yakiyumba kwa miezi kadhaa sasa.
Ikumbukwe kuwa, Machar alikamatwa kwa tuhuma za kujaribu kuchochea uasi mwezi Machi mwaka huu 2015. Mivutano na hali ya wasiwasi imekuwa ikiongezeka kati ya pande mbili za Rais Salva Kiir na Machar na ikashtadi mnamo mwezi Februari mwaka huu wakati kundi liitwalo Jeshi Jeupe ambalo ni tiifu kwa Machar, lilipovamia kambi ya jeshi jimboni la Upper Nile na kushambulia pia helikopta ya Umoja wa Mataifa.