Balozi: Burkina Faso inataka kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na Iran
Balozi wa Burkina Faso mjini Tehran, Mohammadi Kaboureh, amesisitiza umuhimu wa kuimarisha ushirikiano wa kisayansi na Iran, akieleza kuwa ni jambo la msingi kwa maendeleo endelevu ya taifa hilo la Afrika.
Kwa mujibu wa shirika rasmi la habari la Iran, IRNA, Kaboureh amesema: “Maendeleo endelevu bila elimu ni jambo lisilowezekana; tunahitaji utaalamu wa thamani kutoka Iran ili kufikia lengo hilo. Burkina Faso imejizatiti kuimarisha ushirikiano na Iran katika nyanja zote, hasa elimu na sayansi.”
Kauli hiyo ameitoa katika kikao na Mkuu wa Shirika la Masuala ya Wanafunzi, Saeed Habiba, kilichofanyika mjini Tehran.
Kaboureh amesifu juhudi za Iran katika kutoa ufadhili wa masomo kwa wanafunzi wa Burkina Faso, akieleza matumaini kuwa idadi kubwa zaidi ya wanafunzi watanufaika na fursa hiyo.
Kwa upande wake, Habiba amesema: “Burkina Faso ni miongoni mwa nchi rafiki wa Iran. Tuna nia ya kupanua ushirikiano wa kisayansi na diplomasia ya kielimu na taifa hilo.”
Vyuo vikuu vya Iran vinaendelea kuvutia wanafunzi wa kimataifa kutokana na kiwango cha juu cha elimu, hasa katika nyanja za sayansi.
Mwezi Desemba, Mkurugenzi wa Masuala ya Wanafunzi Wasio Wairani katika Wizara ya Sayansi, Utafiti na Teknolojia ya Iran, Fereyd Rahimi Nadaf, alitangaza kuwa wanafunzi wa kimataifa wapatao 90,000 wanajifunza katika vyuo vikuu vya umma vya Iran, Chuo Kikuu cha Kiislamu cha Azad, vyuo vya tiba, na taasisi nyingine za elimu ya juu.
Uwepo huu mkubwa wa wanafunzi wa kimataifa unaonyesha nafasi inayokua ya Iran kama kitovu cha elimu ya juu katika ukanda huu, na inaakisi dhamira yake ya kutoa fursa za elimu zilizo pana na zenye mwelekeo wa kimataifa.