Maandamano makubwa ya kuunga mkono Palestina yawavutia maelfu jijini Nairobi
Maelfu ya Wakenya, wakiwemo Waislamu na Wakristo kwa pamoja wamejitokeza kwa wingi jijini Nairobi kushiriki maandamano na tamasha la mshikamano wa kuunga mkono Palestina, yaliyoandaliwa na kikundi cha 'Kenyans for Palestine' kwa ushirikiano na mashirika kadhaa ya kiraia.
Maandamano hayo ya Jumapili yalijumuisha misafara ya magari, bendera za Palestina, na ujumbe wa kuunga mkono Gaza na harakati za ukombozi wa ardhi za Palestina ambazo zinakaliwa kwa mabavu na utawala wa Kizayuni wa Israel.
Tukio hilo limekuwa ishara adimu ya mshikamano wa wazi nchini Kenya kuhusu mauaji ya kimbari yanayoendelezwa na Israel huko Gaza.
Waandamanaji wakiwemo wanasiasa kama vile Hassan Omar, Katibu Mkuu wa chama tawala UDA, wamekosoa msimamo wa serikali wa kutoegemea upande wowote kuhusu kadhia ya Palestina. Amesema Kenya lazima ijiunge na mataifa mengine yanayounga mkono Palestina na kulaani jinai za utawala wa Israel. Waandaaji wamesema idadi kubwa ya waliohudhuria inaonesha kuongezeka kwa hasira miongoni mwa wananchi kuhusu ukimya mbele ya janga la kibinadamu huko Gaza.
Zaidi ya shilingi milioni 10 za Kenya zilikusanywa katika tukio hilo kupitia mnada na michango ili kusaidia huduma za matibabu kwa Wapalestina.
Tukio hilo pia lilizindua mpango wa kupanda miti kama ishara ya kimazingira na mshikamano wa kimataifa.
Watu kutoka maeneo mbalimbali ya Kenya walihudhuria, na wawakilishi wa mikoa walikabidhi michango yao kwa kamati ya waandaaji.
Waandaaji wamesisitiza kuwa tukio hilo halikuwa la harambee tu, bali ni ujumbe wa wazi: Wakenya wanasimama na Palestina, bila kujali misimamo yao ya kisiasa au kidini.