Rais wa Madagascar afanya mazungumzo licha ya waandamanaji kususia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i131780-rais_wa_madagascar_afanya_mazungumzo_licha_ya_waandamanaji_kususia
Rais Andry Rajoelina wa Madagascar jana aliyaalika makundi na asasi kadhaa za kiraia kwa ajili ya mazungumzo katika ikuu ya Rais.
(last modified 2025-10-09T07:13:48+00:00 )
Oct 09, 2025 07:13 UTC
  • Rais wa Madagascar afanya mazungumzo licha ya waandamanaji kususia

Rais Andry Rajoelina wa Madagascar jana aliyaalika makundi na asasi kadhaa za kiraia kwa ajili ya mazungumzo katika ikuu ya Rais.

Rais wa Madagascar amechukua hatua hiyo katika jitihada za kurejesha mamlaka ya uongozi wake na kupunguza mzozo ulioikumba nchi hiyo kufuatia maandamano ya nchi nzima ambayo yamekuwa yakiendelea tangu tarehe 25 mwezi Uliopita. 

Watu zaidi ya 1,500 jana waliitikia wito wa kukutana na kuzungumza na Rais wakiwemo wawakilishi wa ngazi ya juu wa makanisa, wakuu wa Vyuo VIkuu, wanafunzi, jumuiya za vijana, wajasiriamali, makampuni yaliyoathiriwa na vitendo vya wizi na uporaji, vyama vya wafanyakazi, wafanyakazi wa sekta ya afya na tiba, walimu, wanariadha, wasanii na waandishi wa habari.

Rais Andry Rajoelina amewahakikishia washiriki wa mazungumzo hayo kuwa atajizulu  ikiwa kukatika kwa umeme kutaendelea katika mji mkuu wa Madagascar, Antananarivo katika muda wa mwaka mmoja.

"Naapa mbele ya Mwenyezi Mungu," aliuambia umati. "Nipeni muda wa mwaka mmoja! Nitafaulu!", alisema Rais wa Madagascar mbele ya hadhira iliyoshiriki mazungumzo ikulu jana Jumatano ili kupata suluhu ya mgogoro ulioikumba Madagascar. 

Rais wa Madagascar alikwenda mbali zaidi kwa kusema:" "Tutasafirisha hata (jenereta) kwa ndege ikihitajika, ili kusiwe na uhaba mkubwa umeme katiak mji mkuu Antananarivo na kote Madagascar." 

Maandamano yaliyoongozwa na Gen-Z hivi karibuni yaliikumba Madagascar kufuatia ghadhabu za wananchi waliokuwa wakilamikia uhaba wa maji na umeme.