Upinzani Ethiopia: Serikali iache kuua na kukandamiza waandamanaji
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13228-upinzani_ethiopia_serikali_iache_kuua_na_kukandamiza_waandamanaji
Vyama vya upinzani nchini Ethiopia vimevunja kimya chao na kuitaka serikali ya nchi hiyo kukomesha mauaji na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji.
(last modified 2023-11-27T12:14:11+00:00 )
Aug 14, 2016 06:53 UTC
  • Upinzani Ethiopia: Serikali iache kuua na kukandamiza waandamanaji

Vyama vya upinzani nchini Ethiopia vimevunja kimya chao na kuitaka serikali ya nchi hiyo kukomesha mauaji na ukandamizaji dhidi ya waandamanaji.

Profesa Beyene Petros, mwenyekiti wa muungano wa upinzani wa Medrek ameitaka serikali ya Addis Ababa kuheshimu haki za msingi kama kujumuika na kufanya maandamano ya amani na kubainisha kuwa, watawala wa nchi hiyo wanawauawa na kuwakandamiza waandamanaji kwa lengo la kulinda biashara na mali zao.

Kadhalika mwenyekiti wa muungano wa Medrek wenye vyama vinne vya upinzani ameitaka serikali ya Ethiopia iwaachie huru wafungwa wa kisiasa sambamba na kuwapa fidia familia za wahanga wa ukandamiza wa polisi.

Ukandamizaji wa polisi ya Ethiopia

Haya yanajiri siku chache baada ya Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa kuonyesha wasi wasi mkubwa juu ya kushadidi machafuko katika mkoa wa Oromo na Amhara, kaskazini mwa Ethiopia na kuongeza kuwa, hali hiyo imeathiri pakubwa hali ya kibinadamu katika nchi hiyo ya Pembe ya Afrika. 

Farhan Haq, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa

Duru za habari zimearifu kuwa idadi ya watu waliouawa na polisi miongoni mwa waandamanaji katika mikoa hiyo miwili ya Oromo na Amhara, imepindukia 100.

Shirika la Kutetea Haki za Binadamu linalofungamana na Umoja wa Mataifa limeitaka serikali ya Ethiopia iruhusu kutumwa nchini humo waangalizi wa kimataifa kwa shabaha ya kufanya uchunguzi kuhusiana na mauaji ya hivi karibuni nchini humo.