Rais wa Zambia atangazwa mshindi katika uchaguzi wenye ulalamishi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13327-rais_wa_zambia_atangazwa_mshindi_katika_uchaguzi_wenye_ulalamishi
Rais Edgar Lungu wa Zambia leo ametangazwa mshindi rasmi wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa ushindi mdogo dhidi ya mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema, huku chama cha mgombea huyo wa upinzani kikikataa kuyatambua matokeo hayo na kiutuhumu tume ya uchaguzi kuwa imezitia mkono kura.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 15, 2016 11:49 UTC
  • Rais wa Zambia atangazwa mshindi katika uchaguzi wenye ulalamishi

Rais Edgar Lungu wa Zambia leo ametangazwa mshindi rasmi wa uchaguzi wa rais wa nchi hiyo kwa ushindi mdogo dhidi ya mpinzani wake mkuu Hakainde Hichilema, huku chama cha mgombea huyo wa upinzani kikikataa kuyatambua matokeo hayo na kiutuhumu tume ya uchaguzi kuwa imezitia mkono kura.

Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zambia (ECZ)  Jaji Esau Chulu amemtangaza Edgar Chagwa Lungu kuwa rais mteule kwa kupata asilimia 50.35 ya kura dhidi ya mpinzani wake Hakainde Hichelema aliyepata asilimia 47.63 ya kura zote.

Mkuu wa ECZ Jaji Esau Chulu akitangaza matokeo ya uchaguzi

Katika uchaguzi wa rais uliofanyika mwaka jana kujaza nafasi iliyobaki wazi baada ya aliyekuwa rais wa nchi hiyo Michael Sata kufariki dunia, Lungu alimshinda pia Hichilema kwa kura chache.

Mara baada ya kutangazwa matokeo hayo wafuasi wa Lungu waliovalia sare za chama tawala cha Harakati ya Kizalendo (PF) walimiminika barabarani huku wakiimba na kupiga honi za gari kusherehekea ushindi.

Rais Lungu (kulia) na mpinzani wake Hichilema (kushoto) 

Hata hivyo Chama cha Hichilema cha Muungano kwa ajili ya Maendeleo ya Taifa (UPND) kimeyapinga matokeo hayo kwa kuwatuhumu maafisa wa tume ya uchaguzi kuwa walikula njama kwa maslahi ya Lungu tangu zoezi la kuhesabu kura lilipoanza Alkhamisi usiku na kusisitiza kuwa kitakata rufaa ya kupinga matokeo hayo katika Mahakama ya Katiba.

Wakili wa chama hicho Jack Mwiimbu amewaambia waandishi wa habari kuwa wana ushahidi unaoonyesha kuwa kura za Hakainde Hichilema zilipunguzwa makusudi na tume ya uchaguzi na kusisitiza kwamba wana imani kamili kuwa Mahakama ya Katiba itaukataa uamuzi wa tume na kubatilisha matokeo hayo.../