Global Citizen: Mkutano wa G20 umefikia malengo licha ya mivutano
-
Mkutano wa G20 Afrika Kusini
Afrika Kusini imefikia malengo muhimu katika mkutano wa kilele wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi duniani G20 licha ya mivutano ya kimataifa. Hayo yameelezwa na shirika la hisani la Global Citizen.
Mkutano wa kilele wa siku mbili wa kundi la mataifa tajiri na yale yanayoinukia kiuchumi duniani la G20 umemalizika leo jijini Johannesburg nchini Afrika Kusini na kutoa ishara ya uthabiti. Michael Sheldrick wa Global Citizen amesema: "Licha ya mivutano katika siasa za kilimwengu, lakini mkutano huu wa kilele wa G20 umeonyesha kuwa, ushirikiano wa kimataifa bado unawezekana ikiwa nchi zitawajibika."
Uwenyekiti wa kupokezana wa G20 unaoshikiliwa kwa sasa na Afrika Kusini umefanikiwa kuhamasisha muungano mpana ili kuharakisha upanuzi wa nishati mbadala barani Afrika, alisema Sheldrick. Takriban watu milioni 600 barani Afrika wanaishi bila umeme. Washiriki walipitisha kwa kauli moja taarifa ya mwisho baada ya mazungumzo kugubikwa na mpango wa amani wa Marekani kuhusu mzozo wa Ukraine.
Marekani, mwanachama mwanzilishi wa G20, iliususia mkutano wa mwaka huu. Mapema mwezi huu, Rais wa Marekani Donald Trump alitangaza kuwa hatatuma afisa yeyote wa Marekani Johannesburg, akitoa madai ya “ukiukaji wa haki za binadamu” dhidi ya jamii ya Waafrika wazungu makaburu (Waafrikana), madai ambayo serikali ya Afrika Kusini imeyakanusha mara kwa mara na kusema hayana msingi.
Mwaka huu, uhusiano kati ya Washington na Pretoria umedorora kwa kiwango cha chini zaidi kutokana na tofauti za sera za ndani na za kimataifa hasa hatua ya Pretoria ya kuishtaki Isreal mshirika wa Marekani katika Mahakama ya Kimataifa ya Haki kutokana na jinai zake katika Ukanda wa Gaza.