Malalamiko ya wapinzani nchini Zambia kwa matokeo ya uchaguzi
Viongozi wa chama cha upinzani nchini Zambia cha Muungano kwa Ajili ya Maendeleo ya Taifa (UPND) wamepinga matokeo ya uchaguzi wa Rais na wanasema kuwa, watawasilisha mashtaka katika Mahakama ya Katiba kupinga matokeo ya uchaguzi huo uliofanyika Alkhamisi iliyopita.
Wapinzani hao wanadai kuwa, wana ushahidi unaoonesha kuwa, kulikuweko vitendo vya udanganyifu katika uchaguzi huo. Hata hivyo Davies Chama, Katibu Mkuu wa chama tawala cha Patriotic Front (PF) amewatuhumu wapinzani kwamba, wanatafuta visingizio tu baada ya kushindwa katika kinyang'anyiro cha uchaguzi.
Wakati huo huo, viongozi wa chama kikongwe cha United National Independence Party (UNIP) kilichoasisiwa na Kenneth Kaunda, kiongozi mpigania uhuru wa Zambia nacho kimepinga matokeo ya uchaguzi huo na kina mpango wa kuwasilisha mashtaka mahakamani. Malalamiko na upinzani wa vyama viwili vya kisiasa dhidi ya matokeo ya uchaguzi wa Rais yanaweza kupelekea kufunguliwa faili Edgar Lungu na chama tawala katika vyombo vya mahakama na kumtia matatani kiongozi huyo.
Kwa mujibu wa matokeo ya mwisho yaliyotangazwa na Tume ya Uchaguzi ya Zambia, Rais Edgar Lungu wa chama tawala ameibuka mshindi kwa kujinyakulia asilimia 50.35 ya kura dhidi ya mpinzani wake, Hakainde Hichilema wa chama cha upinzani cha UPND aliyepata asilimia 47.63 ya kura zote. Lungu amemshinda mpinzani wake Hichilema ambaye ni mfanyabiashara tajiri kwa tofauti ya takribani kura laki mbili.
Kwa matokeo hayo, Rais Lungu ataiongoza Zambia kwa kipindi cha miaka mitano. Chama cha upinzani cha Hichilema kinasema kuwa, kucheleweshwa kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo ni moja ya dalili za kufanyika udannganyifu kwa maslahi ya chama tawala.
Hii ni mara ya tano kwa chama cha upinzani cha Muungano kwa Ajili ya Maendeleo ya Taifa (UPND) kushindwa katika uchaguzi wa Rais nchini Zambia.
Akizungumzia matokeo ya uchaguzi huo, Katibu Mkuu wa chama tawala Davies Chama amesema kuwa, kushindwa chama hicho cha upinzani katika uchaguzi wa Alkhamisi ndio mwisho wa harakati za chama hicho katika uga wa siasa za Zambia.
Wakati huio huo huo wachambuzi wa masuala ya kisiasa na kiuchumi wameshangazwa na matokeo ya uchaguzi huo pamoja na ushindi wa Rais Edgar Lungu.
Hii ni kutokana na kuwa, utendaji wa kiongozi huyo katika kipindi cha kumalizia muda wa Rais aliyefariki dunia, Michael Sata haukuwa wa kuridhisha. Kiwango cha ukuaji wa uchumi nchini Zimbabwe kimefikia asilimia 3.6 ambapo kuanzia mwaka 1998 hiki ni kiwango kidogo zaidi cha ukuaji wa uchumi nchini humo. Zambia ina akiba kubwa ya madini ya shaba. Katika miaka ya hivi karibuni nchi hiyo imepata hasara kubwa kutokana na kushuka kwa bei ya madini hayo katika soko la dunia. Kupungua uwekezaji katika sekta ya madini ya shaba ambako kumepelekea maelfu ya vibarua kukosa ajira katika uchimbaji wa madini hayo na wakati huo huo kuongezeka kwa asilimia 20 kiwango cha ughali wa maisha ni ishara za wazi za kudorora uchumi wa Zambia.
Katika mazingira kama haya, baadhi ya wajuzi wa mambo wanaamini kwamba, ushindi wa Edgar Lungu katika uchaguzi wa rais umetokana na ushawishi mkubwa wa chama tawala kati ya wananchi wa Zambia. Lungu ambaye alishika hatamu za uongozi wa Zambia mwaka 2015 katika uchaguzi wa mapema kufuatia kifo cha ghafla cha Michael Sata, naye kama alivyokuwa Sata amefanya juhudi za kujipatia nafasi na ushawishi kwa fikra za waliowengi nchini Zambia.
Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, misimamo na hatua kali za Edgar Lungu kuhusiana na uhuru wa vyombo vya habari, uhuru wa kutoa maoni na vilevile uhuru wa magazeti ni mambo ambayo yamemfanya kiongozi huyo akabiliwe na ukosoaji mkali.
Pamoja na hayo yote, Edgar Lungu ambaye anatoka katika kabila la waliowachache la Nsenga alisisitiza katika kampeni zake za uchaguzi kwamba, atakuwa kiongozi wa Wazambia wote na kwa msingi huo akafanikiwa kuwavutia wapiga kura.