Zaidi ya watu 38 wauawa mashariki mwa Libya
Baraza la Shura ya Wanamapinduzi la Benghazi limetangaza kuwa wapiganaji 38 watiifu kwa Jenerali Khalifa Haftar wameuawa katika mapigano na vikosi vitiifu kwa baraza hilo huko Benghazi mashariki mwa Libya.
Duru za Baraza la Shura ya Wanamapinduzi la Benghazi zimedai pia kuwa katika mapigano hayo yaliyotokea jana wapiganaji wake wamefanikiwa kuyatwaa tena baadhi ya maeneo kutoka mikononi mwa askari watiifu kwa Jenerali Haftar pamoja na silaha na zana za kivita.
Siku ya Jumatatu mtu mmoja aliuawa na wengine watatu walijeruhiwa katika mapigano yaliyotokea baina ya pande hizo mbili. Mapigano hayo yamekita zaidi katika eneo la al-Qawarisha na baadhi ya sehemu za magharibi za mji wa Benghazi.
Imeelezwa kuwa mapigano yalizuka baada ya vikosi vya Jenerali Khalifa Haftar kutaka kusonga mbele kuelekea maeneo yanayodhibitiwa na wapiganaji wa Baraza la Shura ya Wanamapinduzi; hata hivyo mabomu ya ardhini yaliyotegwa na wapiganaji hao yalivizuia vikosi vya Haftar kusonga mbele.
Baada ya kuangushwa utawala wa dikteta Muammar Gadafi mnamo mwaka 2011, Libya imegawika sehemu mbili za mshariki na magharibi. Huko magharibi mwa nchi kuna Serikali ya Makubaliano ya Kitaifa (GNA) inayoongozwa na Baraza la Urais chini ya uongozi wa Waziri Mkuu Fayaz al-Siraj na amabyo ndiyo inayotambuliwa na Jamii ya Kimataifa; na upande wa mashariki kuna serikali iliyoundwa na jenerali mstaafu wa jeshi la Libya Khalifa Haftar.../