Mamia waandamana Mogadishu kumlaani Trump kwa kuwatukana Wasomali
-
Mamia waandamana Mogadishu kumlaani Trump kwa kuwatukana Wasomali
Mamia ya watu wamemiminika mitaani huko Mogadishu mji mkuu wa Somalia kuonesha hasira zao dhidi ya rais wa Marekani Donald Trump aliyewatukana Wasomali na kuwaita "takataka."
Akizungumza katika mkutano wa baraza la mawaziri Jumanne, Trump alisema Wamarekani wenye asili ya Somalia "hawachangii chochote," "Hatuwataki katika nchi yetu na ni takataka tu."
Matusi ya rais huyo wa Marekani yamepokewa kwa mshtuko na kulaaniwa ndani ya Marekani na nje ya Marekani hasa nchini Somalia.
"Tunapinga maneno ya matusi ya Trump akituita sisi ni takataka," amesema Ridwan Mohamud katika maandamano huko Mogadishu. "Sisi si takataka. Yeye ndiye takataka kwa mdomo wake mchafu. Kwa kuwa ameshindwa katika siasa zake, sasa anajaribu kupotosha umma."
Kuna zaidi ya watu robo milioni wenye asili ya Somalia wanaoishi Marekani, akiwemo Mbunge wa chama cha Democratic Ilhan Omar ambaye mara kwa mara anakosoa sera za kibaguzi na Donald Trump.
Waandamanaji wamebeba mabango na picha za mbunge Ilhan Omar na kutangaza kwa sauti kubwa kaulimbiu za kumlaani Trump.
"Trump amekiuka heshima na utu wetu na hatukubali kutukanwa," amesema, mwandamanaji mwingine, Fadumo Ahmed, na kuongeza kuwa: "Sisi ni Wasomali, na tuna fakhari yetu wenyewe. Lakini mtu kama Trump hana elimu ya kuelewa hilo."
Matusi ya Trump dhidi ya Wamarekani wenye asili ya Somalia yamelaaniwa vikali kila sahemu, hata Gavana wa Minnesota, Tim Walz na viongozi wengine wa majimbo wamelaani matusi hayo ya Trump.