Ukosefu mkubwa maji unazidi kusambaa kusini mwa Somalia
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134084-ukosefu_mkubwa_maji_unazidi_kusambaa_kusini_mwa_somalia
Vyanzo muhimu vya maji kusini mwa Somalia vinakauka kwa kasi huku ukame ukiongezeka, na kusababisha uhaba mkubwa kwa mamia ya maelfu ya watu.
(last modified 2025-12-09T02:38:56+00:00 )
Dec 09, 2025 02:38 UTC
  • Ukosefu mkubwa maji unazidi kusambaa kusini mwa Somalia

Vyanzo muhimu vya maji kusini mwa Somalia vinakauka kwa kasi huku ukame ukiongezeka, na kusababisha uhaba mkubwa kwa mamia ya maelfu ya watu.

Katika Jimbo la Jubaland, hali ni ya kutisha zaidi katika wilaya za Baardheere, Belet-Xaawo, Ceel Waaq, Doolow, Garbahaarey na Luuq, mkoa wa Gedo. Mamlaka za Jubaland zinasema zaidi ya watu 570,000 wanakabiliwa na upungufu mkubwa wa maji, watu 213,300 katika wilaya sita za Gedo, takribani watu 257,000 katika mkoa wa Lower Juba, na zaidi ya watu 100,000 katika mkoa wa Middle Juba. Idadi hii inatarajiwa kuongezeka kadri vyanzo vya maji vinavyoendelea kukauka.

Hali ya dharura hii imetokana na mvua duni za msimu wa Aprili–Juni na kukosekana kabisa kwa mvua za Oktoba–Desemba. Mfululizo wa mishtuko ya mabadiliko ya hali ya hewa, ukichangiwa na upungufu wa ufadhili, umezuia kwa kiasi kikubwa msaada kuwafikia waathirika.

Familia zinalazimika kutembea umbali mrefu kutafuta maji, na pale yanapopatikana kibiashara, gharama zake huwa ghali na wengi hawazimudu. Mamlaka za Jubaland zimetoa wito wa msaada wa dharura ili kuzuia kuporomoka kwa maisha ya wakulima na wafugaji, na kupunguza vifo vinavyoweza kuepukika.

Wameonya kuwa miezi minne ijayo itakuwa ya maamuzi, kwani mvua inayofuata inatarajiwa tu Aprili 2026. Tayari katika eneo la Middle Juba, mvutano kati ya jamii mbali mbali unaripotiwa kutokana na uhaba wa malisho na maji.