Mlipuko wa kipindupindu DRC umeua watu 1,888, wakiwemo watoto 340
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134094-mlipuko_wa_kipindupindu_drc_umeua_watu_1_888_wakiwemo_watoto_340
Mlipuko wa kipindupindu mwaka huu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeleta madhara makubwa, ukiwa na jumla ya wagonjwa 64,427 tangu mwanzo wa mwaka huu 2025, na kusababisha vifo 1,888. Watoto waliougua ni 14,818 na waliofariki dunia ni 340, na hivyo kufanya huu kuwa mlipuko mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25 nchini humo. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF linaeleza.
(last modified 2025-12-09T07:24:24+00:00 )
Dec 09, 2025 07:24 UTC
  • Mlipuko wa kipindupindu DRC umeua watu 1,888, wakiwemo watoto 340

Mlipuko wa kipindupindu mwaka huu nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) umeleta madhara makubwa, ukiwa na jumla ya wagonjwa 64,427 tangu mwanzo wa mwaka huu 2025, na kusababisha vifo 1,888. Watoto waliougua ni 14,818 na waliofariki dunia ni 340, na hivyo kufanya huu kuwa mlipuko mbaya zaidi katika kipindi cha miaka 25 nchini humo. Hayo ni kwa mujibu wa Shirika la Umoja wa Mataifa la Kuhudumia Watoto, UNICEF linaeleza.

Mlipuko huu umevuruga elimu ya watoto, ukiwaweka kwenye hatari ya kuugua na kushuhudia mateso na vifo vya wanafamilia. Katika tukio la kusikitisha zaidi, watoto 16 kati ya 62 wanaoishi katika kituo cha kulelea watoto yatima huko Kinshasa walifariki ndani ya siku chache baada ya ugonjwa huo kusambaa katika nyumba hiyo ya malezi.

John Agbor, Mwakilishi wa UNICEF nchini DRC amesema. “Watoto wa DRC hawapaswi kuathiriwa kwa kiwango kikubwa kiasi hiki na ugonjwa ambao unaweza kuzuilika kabisa."

Agbor anaendelea kwamba, “UNICEF inahimiza serikali kuongeza uwekezaji katika huduma za maji, usafi wa mazingira, usafi wa mwili na huduma za afya, hususan katika maeneo yanayojulikana kuwa na mlipuko wa kipindupindu ili kulinda afya na ustawi wa familia na watoto wa DRC.”

Majimbo 17 kati ya 26 ya DRC yameathirika kwa sasa, ikiwemo mji mkuu Kinshasa. Asilimia ya watoto katika mlipuko hutofautiana kulingana na mkoa, lakini wastani kitaifa ni takriban asilimia 23.4.

Upatikanaji mdogo wa huduma za maji safi na usafi wa mazingira unaendelea kuchochea kuendelea kwa kipindupindu nchini DRC.

Serikali ya DRC imeandaa mpango wa kitaifa wa kutokomeza kipindupindu, unaojulikana kama Mpango wa Sekta Nyingi wa Kutokomeza Kipindupindu (PMSEC) 2023–2027, wenye bajeti ya dola milioni 192. Hata hivyo, mpango huu unakabiliwa na upungufu mkubwa wa fedha, na tathmini ya muda wa kati iliyokamilishwa Mei 2025 imependekeza kuongezwa kwa uwekezaji na uratibu madhubuti wa sekta mbalimbali.

Kufuatia mlipuko wa 2025, serikali pia imeanzisha mpango wa “Mto Congo bila kipindupindu” ili kushughulikia ukosefu wa hatua za kudhibiti kipindupindu katika bandari, kutokuwa na mpango wa usafi kwa boti, kukosa uelimishaji kwa wahudumu na abiria, pamoja na upatikanaji wa maji safi ya kunywa kando ya mto.