Rais wa DRC aituhumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya 'amani' yaliyofikiwa Marekani
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i134096-rais_wa_drc_aituhumu_rwanda_kwa_kukiuka_makubaliano_ya_'amani'_yaliyofikiwa_marekani
Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, ameituhumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya 'amani' yaliyosimamiwa na Marekani na kutiwa saini wiki iliyopita mjini Washington DC.
(last modified 2025-12-09T09:08:03+00:00 )
Dec 09, 2025 07:26 UTC
  • Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi
    Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, ameituhumu Rwanda kwa kukiuka makubaliano ya 'amani' yaliyosimamiwa na Marekani na kutiwa saini wiki iliyopita mjini Washington DC.

Makubaliano hayo, yaliyosimamiwa na Rais Donald Trump, yamekosolewa vikali na wachambuzi wengi wanaosema yamelenga zaidi kurahisisha uhamishaji wa madini adimu kutoka mashariki mwa DRC kuliko kuleta amani ya kweli katika eneo hilo. Trump mwenyewe amesema baada ya mapatano hayo makampuni ya kiteknolojia ya Marekani yataweza kuchimba madini ya DRC, jambo linaloweka wazi nia yake ya kupora madini ya nchi hiyo.

Akihutubia bunge Jumatatu, Tshisekedi alisema: “Rwanda tayari inakiuka ahadi zake.” Alifafanua kuwa siku moja tu baada ya kutiwa saini kwa makubaliano hayo tarehe 4 Desemba, jeshi la Rwanda lilifyatua silaha nzito kutoka mji wa Bugarama kuelekea Congo, na kusababisha uharibifu mkubwa wa mali na maisha katika maeneo ya Kaziba, Katogota na Lubarika, jimbo la Kivu Kusini.

Amesema makubaliano hayo yanataka Rwanda kuondoa mara moja majeshi yake mashariki mwa Congo, kuvunja makundi ya kigeni yenye silaha ikiwemo waasi wa FDLR, kusitisha mapigano na kuanzisha chombo cha usalama cha pamoja cha kusimamia utekelezaji.

Kwa miongo kadhaa, eneo la mashariki mwa Congo limekumbwa na ghasia zilizoua maelfu na kusababisha mamilioni ya watu kuwa wakimbizi.

Mapigano kati ya waasi wa M23 na jeshi la serikali yaliendelea Jumatatu katika eneo la Masisi, jimbo la Kivu Kaskazini, huku pande zote zikilaumiana. Waasi wa M23 walijitokeza tena mwaka 2021 na kuanzisha mashambulizi makali dhidi ya vikosi vya serikali.

Rwanda inatuhumiwa na DRC pamoja na Umoja wa Mataifa kwa kuunga mkono M23, madai ambayo Kigali imekanusha.

Wakati huohuo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Burundi, Edouard Bizimana, ametuhumu Rwanda kwa kuendeleza “harakati za kuvuruga usalama” mpakani na DRC. Amesisitiza kuwa majeshi ya Burundi yaliyotumwa mashariki mwa DRC hayataondoka hadi “jukumu lao litakapokamilika kikamilifu.” Takribani askari 15,000 wa Burundi wameripotiwa kuwa mashariki mwa DRC wakisaidia jeshi la nchi hiyo kupambana na waasi.

Kwa upande wake, serikali ya Rwanda imeituhumu Burundi na Rais wake Évariste Ndayishimiye kwa kuchochea mgawanyiko miongoni mwa wananchi wa Rwanda.