Kupigwa marufuku maandamano dhidi ya serikali nchini Ethiopia
Polisi nchini Ethiopia imepiga marufuku maandamano ya aina yoyote ile ya kuipinga serikali ya nchi hiyo.
Mkuu wa Muungano wa upinzani (MEDREK) nchini Ethiopia ametangaza kuwa, vikosi vya polisi vimepelekwa katika miji ya Oromia na Amhara kaskazini mwa nchi hiyo ili kuzuia maandamano yanayopinga serikali ya nchi hiyo.
Juma lililopita miji hiyo ilishuhudia kwa mara ya kwanza mikusanyiko iliyofanyika kwa wakati mmoja ili kuonyesha upinzani dhidi ya serikali. Maandamano dhidi ya serikali huko Oromia na Amhara yanashadidi katika hali ambayo, hitilafu za kikaumu na kiutamaduni zinaripotiwa kuongezeka nchini Ethiopia.
Wimbi la maandamano dhidi ya serikali ya Ethiopia lilianza Disemba mwaka jana baada ya serikali kuanza kutekeleza mpango wa kupanua mji mkuu Addis Ababa kuelekea upande wa Oromia. Wakulima wa mji huo wanaamini kwamba, mpango huo wa serikali wa kuupanua mji wa Addis Ababa una maana ya kupora ardhi za wakulima na wakiwa na lengo la kupinga mpango huo walianza kumiminika barabarani na kuandamana.
Viongozi wa kaumu za Oromo na Amhara wanaituhumu serikali ya Ethiopia kwamba, imekuwa ikiwabagua na kutoa upendeleo kwa kaumu ya Tigre. Katika asasi za serikali, mashirika ya kiintelijensia na vyombo vya usalama kunashuhudiwa kwa wingi watu wa kabila la Tigre wakiwa wanashika nyadhifa mbalimbali. Wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, Ubaguzi wa kisiasa na kijamii unaofanywa dhidi ya makabila hayo ndio uliopelekea kulipuka ghadhabu kubwa miongoni mwa watu wa makabila hayo.
Shirika la Kutetea Haki za Binadamu la Human Rights Watch limetangaza kuwa, malalamiko ya wananchi ya wiki iliyopita nchini Ethiopia huko Oromia na Amhara yalikandamizwa na vikosi vya usalama ambapo kwa uchache watu mia moja waliuawa katika tandabelua hilo.
Machafuko nchini Ethiopia yanaendelea katika hali ambayo, Naibu Msemaji wa Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema kuwa, kushadidi vita katika eneo hilo kumeifanya hali ya kibinadamu na haki za binadamu nchini Ethiopia kuwa mbaya zaidi ikilinganishwa na hapo kabla na hivyo kuyafanya matatizo ya nchi hiyo kuwa maradufu.
Farhan Haq ameongeza kuwa, Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa ana wasiwasi mkubwa kutokana na kuongezeka mivutano kati ya pande mbili katika miji ya Oromia na Amhara nchini Ethiopia pamoja na utumiaji mabavu uliofanywa na vikosi vya usalama dhidi ya raia katika siku za hivi karibuni kwenye maeneo hayo.
Kushadidi ukandamizaji wa vikosi vya usalama dhidi ya wapinzani wa serikali nchini Ethiopia ulilifanya Shirika la Kutetea Haki za Binadamu linalofungamana na Umoja wa Mataifa wiki iliyopita, liitake serikali ya Addis Ababa iruhusu kutumwa nchini humo waangalizi wa kimataifa kwa shabaha ya kufanya uchunguzi kuhusiana na mauaji ya hivi karibuni nchini humo.