Maandamano ya upinzani DRC yaanza bila kishindo, wapinzani wakamatwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1351-maandamano_ya_upinzani_drc_yaanza_bila_kishindo_wapinzani_wakamatwa
Polisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inawazuilia wanaharakati 6 wa nchi hiyo ambao wanaaminika kuwachochea wananchi wajitokeze kwa wingi katika maandamano ya leo ya kumshinikiza Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kujiuzulu wadhifa wake atakapomaliza muhula wake Disemba mwaka huu.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 16, 2016 04:43 UTC
  • Maandamano ya upinzani DRC yaanza bila kishindo, wapinzani wakamatwa

Polisi katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inawazuilia wanaharakati 6 wa nchi hiyo ambao wanaaminika kuwachochea wananchi wajitokeze kwa wingi katika maandamano ya leo ya kumshinikiza Rais Joseph Kabila wa nchi hiyo kujiuzulu wadhifa wake atakapomaliza muhula wake Disemba mwaka huu.

Wanaharakati hao walikamatwa usiku wa kuamkia leo katika mji wa Goma ulioko mashariki wa nchi hiyo ya Afrika ya Kati. Hadi tunaenda mitamboni, maandamano hayo ya mjini Kinshasa na maeneo mengine ya DRC yalikuwa hayajashika kasi. Awali, Kiongozi mkuu wa chama cha upinzani (ECiDé), Martin Fayulu alitiwa mbaroni na askari wa usalama mjini Kinshasa, mji mkuu wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo. Taarifa zinasema kuwa, Fayulu alitiwa mbaroni Jumapili jioni mbele ya ofisi yake mjini Kinshasa na kupelekwa kusikojulikana na maafisa usalama wa nchi hiyo. Kabla ya hapo Martin Fayulu alikuwa amewataka raia wa nchi hiyo kushiriki kwa wingi katika maandamano ya leo Februari 16 kwa ajili ya kuishinikiza serikali kuhakikisha uchaguzi mkuu ujao unafanyika katika tarehe iliyopangwa kwa mujibu wa katiba na kuheshimu katiba ya nchi hiyo. Kwa mujibu wa katiba, Rais Joseph Kabila haruhusiwi kugombea tena katika uchaguzi ujao. Hata hivyo wadadisi wa mambo wanaamini kuwa, kama walivyo viongozi wengi wa Kiafrika, rais huyo hayuko tayari kuachia madaraka nchini humo.