Kuongezeka mivutano ya kisiasa nchini Uganda sambamba na kukaribia kufanyika uchaguzi
Sambamba na kukaribia kufanyika uchaguzi mkuu nchini Uganda hapo keshokutwa Alkhamisi, nchi hiyo inashuhudia kuongezeka mivutano ya kisiasa.
Jumatatu ya jana polisi ya Uganda ilimtia mbaroni na kisha kumuachilia huru Dakta Kizza Besigye mmoja wa wagombea urais katika uchaguzi ujao mwanasiasa ambaye anahesabiwa kuwa mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni. Besigye ambaye anagombea urais kupitia chama cha Jukwaa Kwa Ajili ya Mabadiliko ya Kidemokrasia (FDC) alikamatwa na polisi wakati alipokuwa akielekea kwenye mkutano wa hadhara katika wilaya yenye shughuli nyingi, jijini Kampala. Jeshi la Polisi lilidai kuwa lilimkamata Besigye baada ya kukaidi amri ya polisi ya kumtaka atumie barabara nyingine kwa ajili ya kuelekea Kampala. Besigye kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda amewahi kugombea Urais mara tatu na mara zote ameshindwa. Hata hivyo wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, uchaguzi wa Rais mara hii nchini Uganda una tofauti na chaguzi zilizotangulia kutokana na mabadiliko yaliyotokea katika anga ya kisiasa ya nchi hiyo ya mashariki mwa Afrika. Mbali na Museveni na Besigye, kuna wagombea wengine sita ambao nao wamejitokeza kuwania kiti hicho cha Urais akiwemo Amama Mbabazi aliyewahi kuwa Waziri Mkuu na mtu wa karibu wa Rais Museveni.
Katika kampeni zake za uchaguzi, Amama Mbabazi ameahidi kwamba, endapo atachaguliwa na kushika hatamu za Uganda ataweka ukomo wa uongozi wa Rais.
Jumatatu ya jana, Umoja wa Afrika ulitangaza kuwa, timu ya waangalizi 40 inayoongozwa na Sophia Akuffo, mjumbe wa Mahakama Kuu ya Ghana na waangalizi wa Umoja wa Afrika watasimamia mwenendo wa uchaguzi, zoezi la kuhesabu kura na kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo. Rais Museveni ambaye ana umri wa miaka 71 amekuwa madarakani nchini Uganda kwa miaka 30 sasa. Mwaka 2005 Museveni alibadilisha katiba ya nchi na kufuta ukomo wa duru mbili kwa rais na hivyo kujifungulia njia ya kuendelea kubakia madarakani. Museveni ambaye amekuwa madarakani nchini Uganda tangu mwaka 1986 anahesabiwa kuwa, mmoja wa viongozi wakongwe barani Afrika. Wakosoaji wa Rais Museveni wanamtuhumu kwamba, anafanya njama za kutaka kuwa Rais wa milele wa nchi hiyo na kwamba, amekuwa akimuandaa pia mwanawe ili aje kuwa mrithi wake. Wapinzani hao wanasema kuwa, kubadilishwa Katiba na kuondondolewa kikomo cha rais ni hatua moja mbele kuelekea lengo hilo. Aidha wakosoaji wa Rais Museveni wanamtuhumu kwamba, amebinya uhuru wa kisiasa na utawala wake kuwa tishio kwa uhuru wa magazeti.
Kwa upande wao wanaharakati wa Uganda wanatahadharisha kuhusiana na kukabiliwa na tishio uhuru wa magazeti hasa baada ya kufungwa Radio ya Independent. Radio hiyo ilifungwa tarehe 20 mwezi uliopita siku moja tu baada ya kurusha hewani mahojiano ya Amama Mbabazi mgombea urais wa upinzani. Wanaharakati wa masuala ya haki za binadamu sambamba na kutahadharisha kuhusiana na kuwa mbaya hali ya sasa sanjari na kukaribia uchaguzi wanasema kuwa, tangu mwezi Oktoba mwaka jana hadi sasa, zaidi ya waandishi wa habari 40 wametiwa mbaroni na vitendea kazi vyao kuzuiliwa. Kadhalika watatu kati ya waandishi habari hao wameuliwa na kikosi cha polisi. Mwenendo huo ndio unaowafanya weledi wa mambo wawe na wasiwasi wa kuongezeka mvutano wa kisiasa katika nchi hiyo ya Afrika Mashariki.