Kizza Besigye kiongozi mkongwe wa upinzani Uganda yuko mahututi
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i135748-kizza_besigye_kiongozi_mkongwe_wa_upinzani_uganda_yuko_mahututi
Imeelezwa kuwa, hali ya kiafya ya Daktari Kizza Besigye, kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda imezidi kuwa mbaya.
(last modified 2026-01-22T03:07:47+00:00 )
Jan 22, 2026 03:07 UTC
  • Kizza Besigye kiongozi mkongwe wa upinzani Uganda
    Kizza Besigye kiongozi mkongwe wa upinzani Uganda

Imeelezwa kuwa, hali ya kiafya ya Daktari Kizza Besigye, kiongozi mkongwe wa upinzani nchini Uganda imezidi kuwa mbaya.

Taarifa iliyotolewa na chama chake imesema: Afya ya mwanasiasa mkongwe wa upinzani nchini Uganda Kizza Besigye "imefikia hali mbaya", baada ya kupelekwa kwenye kituo cha matibabu katika mji mkuu, Kampala.

Mwanasiasa huyo mwenye umri wa miaka 69 alikimbizwa katika kituo cha matibabu cha kibinafsi chini ya "ulinzi mkali", chama cha People's Front for Freedom (PFF) kilisema, bila kutaja anasumbuliwa na nini.

Hata hivyo, wakuu wa magereza walikanusha kuwa afya ya Besigye ilikuwa mbaya, na kuelezea ziara yake ya usiku kwa daktari kama "uchunguzi wa jumla".

Besigye, daktari wa zamani wa Rais Yoweri Museveni na mmoja wa wapinzani wake wa muda mrefu wa kisiasa, amekuwa kizuizini tangu Novemba 2024.

Kiongozi huyo wa PFF alishtakiwa katika mahakama ya kijeshi kwa kosa la uhaini, ambalo hukumu yake ni kifo, pamoja na kumiliki bunduki kinyume cha sheria na kutishia usalama wa taifa.

Besigye, ambaye amewania urais dhidi ya Museveni mara nne, amekuwa kizuizini na mshirika wake Obeid Lutale tangu wote wawili walikamatwa nchini Kenya na kurudishwa Uganda.

Winnie Byanyima, mke wa Kizza Besigye amewalaumu Rais mteule Yoweri Museveni na mtoto wake wa kiume Jenerali Muhoozi Kainerugaba kwa kile alichokitaja kama kumuweka kizuizini kiharamu na kumyanyasa mumewe kwa kupinga mpango wa urithi wa urais.