Mafuriko mabaya zaidi yaikumba Msumbiji na kusababisha maafa
-
Mafuriko makubwa yaikumba Msumbiji
Watu wasiopunguwa 114 wamefariki dunia na uharibifu mkubwa wa mali umeripotiwa nchini Msumbiji huku baadhi ya vijiji vikifunikwa kabisa na mafuriko yaliyosababishwa na mvua kubwa nchini humo.
Timu ya waokoaji nchini Msumbiji inaendelea kutafuta watu walionusurika baada ya mafuriko mabaya kuwahi kuikumba nchi hiyo. Mamlaka husika zinasema kuwa, takriban watu 114 wameaga dunia tangu ulipoanza msimu wa mvua mwanzoni mwa mwezi Oktoba mwaka jana.
Umoja wa Mataifa umesema kuwa, maji yanayoongezeka yamesababisha hali ya dharura. Katika mkoa wa Kusini mwa Maputo timu ya msaada wa dharura imetembelea eneo kubwa lililofunikwa kabisa na maji ikiwatafuta wakaazi waliokwama pamoja na kutathmini uharibifu uliotokea.
Mkuu wa Ofisi ya Umoja wa Mataifa ya Kuratibu Misaada ya Kibinadamu, OCHA nchini Msumbiji amesema, mafuriko makubwa yaliyosababishwa na mvua zinazoendelea kunyesha, yamesababisha majanga makubwa kwa maisha na mbinu za kujipatia kipato nchini humo, yakiongeza pia hatari ya mripuko wa magonjwa na kuyaweka maeneo ya mijini katika hatari ya kuzingirwa na mamba.
Akizungumza kutoka mji mkuu wa jimbo la Gaza, Xai Xai, Paola Emerson amesema, zaidi ya watu nusu milioni wameathiriwa vibaya na mafuriko hayo, yaliyosababishwa na mvua kubwa katika wiki za mwanzo za mwaka mpya.
“Idadi inaendelea kuongezeka huku mafuriko makubwa yakiendelea na mabwawa yakiendelea kuachilia maji ili kuepuka kupasuka,” ameeleza afisa huyo wa UN na kuongezea kwa kusema: “asilimia 90 ya wananchi wa Msumbiji wanaishi katika nyumba zilizojengwa kwa matofali ya udongo, ambazo kimsingi huweza kumomonyoka baada ya siku chache za mvua”.