Makamu mpya wa Rais wa Sudan Kusini afanya safari nchini Sudan
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i13726-makamu_mpya_wa_rais_wa_sudan_kusini_afanya_safari_nchini_sudan
Makamu mpya wa Rais wa Sudan Kusini jana Jumapili alianza safari ya siku mbili ya kuitembelea Sudan ikiwa ni safari yake ya kwanza mjini Khartoum tangu ateuliwe kushika wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Riek Machar.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Aug 21, 2016 23:27 UTC
  • Makamu mpya wa Rais wa Sudan Kusini afanya safari nchini Sudan

Makamu mpya wa Rais wa Sudan Kusini jana Jumapili alianza safari ya siku mbili ya kuitembelea Sudan ikiwa ni safari yake ya kwanza mjini Khartoum tangu ateuliwe kushika wadhifa huo uliokuwa ukishikiliwa na Riek Machar.

Kamaldeen Ismail, Waziri Mshauri Katika Masuala ya Kigeni wa Sudan amewaambia waandishi wa habari mjini Khartoum Sudan kwamba, serikali ya nchi hiyo imemkubali makamu huyo mpya wa Rais Salva Kiir.

Jana Taban Deng Gai alitarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Bakri Hassan Saleh Makamu wa Kwanza wa Rais wa Sudan.

Aidha leo Makamu huyo wa rais wa Sudan Kusini anatarajiwa kukutana na kufanya mazungumzo na Rais Omar Hassan al-Bashir.

Riek Machar hasimu wa kisiasa wa Rais Salva Kiir

Imeelezwa kuwa, safari ya Makamu huyo wa Rais wa Sudan Kusini huko Khartoum ina lengo la kufanya mazungumzo na viongozi wa nchi hiyo jirani kuhusiana na masuala yaliyobakia yanayozihusu nchi hizo ambapo tangu Sudan Kusini ijitenge na Sudan kumekuweko na masuala ambayo pande hizo zinapaswa kufikia makubaliano.

Hii ni katika hali ambayo, katika mkutano wa hivi karibuni wa Jumuiya ya Igad uliofanyika mjini Kigali Rwanda  viongozi wa jumuiya hiyo walipinga uamuzi wa Rais Salva Kiir wa kumfuta kazi Riek Machar na kumteua Taban Deng Gai.

Wakimbizi wa Sudan Kusini

Riek Machar aliukimbia mji wa Juba baada ya kushadidi mapigano kati ya wafuasi wake na vikosi vya jeshi la serikali mwanzoni mwa mwezi huu wa Julai. 

Baada ya machafuko hayo Rais Salva Kiir alimfuta kazi makamu wake huyo na kumteua Jenerali Taban Deng Gai kushika wadhifa huo.