Ebola yaibuka tena nchini DRC, WHO yaimarisha hatua za kukabiliana na mlipuko
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i138392-ebola_yaibuka_tena_nchini_drc_who_yaimarisha_hatua_za_kukabiliana_na_mlipuko
Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuisaidia kikamilifu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC baada ya kuthibitishwa kwa mlipuko mpya wa ugonjwa hatari wa Ebola katika jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.
(last modified 2026-05-16T03:00:34+00:00 )
May 16, 2026 02:55 UTC
  • Kirusi cha Ebola
    Kirusi cha Ebola

Shirika la Afya Duniani, WHO, limetangaza kuisaidia kikamilifu Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC baada ya kuthibitishwa kwa mlipuko mpya wa ugonjwa hatari wa Ebola katika jimbo la Ituri, kaskazini mashariki mwa nchi hiyo.

Akizungumza mjini Geneva, Uswisi, Ijumaa hii, Mkurugenzi Mkuu wa WHO, Dkt. Tedros Adhanom Ghebreyesus amesema tayari amefanya mazungumzo na Waziri wa Afya wa DRC, Roger Kamba, kuhusu hatua za kukabiliana na mlipuko huo.

Kwa mujibu wa Dkt. Tedros, hadi sasa visa 13 vya Ebola vimethibitishwa na Taasisi ya Kitaifa ya Utafiti wa Tiba ya Kibayolojia, INRB, iliyoko Kinshasa. Amesema WHO ilipokea taarifa za awali za wagonjwa wanaoshukiwa kuwa na Ebola tarehe 5 Mei na mara moja ikatuma timu ya wataalamu katika jimbo la Ituri kusaidia uchunguzi na ukusanyaji wa sampuli.

Ingawa vipimo vya awali vilivyofanyika katika eneo la tukio vilionesha matokeo hasi, baadhi ya sampuli zilizotumwa baadaye Kinshasa zimethibitishwa kuwa na maambukizi ya virusi vya Ebola.

Dkt. Tedros amesema huu ni mlipuko wa 17 wa Ebola kuripotiwa nchini DRC tangu virusi hivyo vilipogunduliwa kwa mara ya kwanza mwaka 1976, akibainisha kuwa nchi hiyo ina uzoefu mkubwa katika kudhibiti na kukabiliana na milipuko ya ugonjwa huo.

Kwa sasa wataalamu wa WHO wanafanya kazi kwa karibu na mamlaka za afya za DRC katika jimbo la Ituri ili kuimarisha hatua za kudhibiti mlipuko huo. Wataalamu zaidi wa mawasiliano ya hatari, ushirikishwaji wa jamii, udhibiti wa maambukizi, huduma za kliniki pamoja na usafirishaji wa vifaa wanatarajiwa kujiunga na juhudi hizo katika siku zijazo.

Aidha, WHO imetuma vifaa vya tiba na vifaa vya kujikinga dhidi ya maambukizi katika mji wa Bunia, makao makuu ya jimbo la Ituri, kusaidia kudhibiti kuenea kwa ugonjwa huo.

Dkt. Tedros pia ametangaza kutolewa mara moja kwa dola za Marekani laki tano kutoka Mfuko wa Dharura wa WHO ili kusaidia kuimarisha mwitikio dhidi ya mlipuko huo.

WHO imesisitiza kuwa itaendelea kushirikiana kwa karibu na serikali ya DRC pamoja na wadau wengine katika eneo hilo ili kudhibiti kuenea kwa virusi vya Ebola na kuhakikisha walioathirika wanapata huduma zinazohitajika.