Indhari kuhusiana na kuenea upenyaji wa Boko Haram barani Afrika
Mratibu wa Kituo cha Taifa cha Upashaji Habari cha Nigeria ametahadharisha kuhusiana na hatari ya kuzidi kujitanua kundi la Boko Haram barani Afrika.
Mike Omer amesema kuwa, hali ya mambo katika maeneo ya kaskazini mashariki mwa Nigeria hususan mji wa Maiduguri ambao ni makao makuu ya jimbo la Borno ni ya hatari sana na ya kusikitisha. Mratibu huyo wa Kituo cha Taifa cha Upashaji Habari cha Nigeria ametahadharisha kuwa, kuenea harakati za kundi la Boko Haram barani Afrika ni jambo hatari sana na kwamba, iwapo wakuu wa nchi za Afrika hawatakaa chini na kulitafutia ufumbuzi jambo hili, basi linaweza kuwa na athari mbaya na hatari sana kwa nchi mbalimbali barani humo. Wachambuzi wa mambo wanasema kuwa, katika kipindi cha miezi kadhaa iliyopita, kundi la kigaidi la Boko Haram limeshadidisha mashambulio yake nchini Nigeria na katika nchi jirani za Cameroon na Niger. Katika shambulio la hivi karibuni kabisa la Boko Haram katika vijiji viwili kaskazini mashariki mwa Nigeria watu wasiopungua 30 waliuawa na wengine wengi kujeruhiwa. Kushadidi duru mpya ya mashambulio ya Boko Haram kunatilia shaka kauli ya Rais Muhammad Buhari wa nchi hiyo kwamba, vikosi vya nchi hiyo vimelishinda kundi hilo. Kiujumla inaonekana kuwa, viongozi wa Nigeria hawana azma ya kweli ya kulitokomeza kundi la Boko Haram. Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kuwa, kushtadi harakati za makundi ya kigaidi kama Boko Haram sio tu ni natija ya udhaifu wa viongozi wa nchi za Kiafrika ikiwemo Nigeria, bali kunatokana pia na kubadilika siasa za kikoloni na kuingizwa nchi kama Saudi Arabia na utawala wa Kizayuni wa Israel katika medani hii. Uchunguzi unaonesha kuwa, utawala wa Kizayuni wa Israel ukiwa na utendaji na mkakati mpya umekuwa ukifanya njama za kupenya na kuwa na ushawishi kwa namna tofauti katika nchi za bara la Afrika.
Nchi ambazo nyingi kati ya hizo licha ya kuwa na utajiri mkubwa kama wa mafuta, madini na gesi lakini zinakabiliwa na hali mbaya ya uchumi na mivutano ya kisiasa. Kutokana na Israel kwa sasa kutengwa kisiasa katika Mashariki ya Kati, inaonekana kuwa, utawala huo ghasibu unafanya harakati za kuwa na ushawishi zaidi barani Afrika kupitia mikataba ya kibiashara na misaada ya kijeshi.
Baadhi ya wachambuzi wa mambo wanaamini kwamba, kuimarika makundi ya kigaidi ni natija ya siasa kama hizi ambapo madola hayo kwa kuyapatia misaada ya kifedha na kijeshi makundi hayo ya kigaidi huchochea moto wa hitilafu kwa ajili ya kufikia malengo yao. Katika uwanja huo baadhi ya nchi za Kiarabu nazo zimekuwa pamoja na madola hayo. Filihali, Saudi Arabia ni nchi ambayo inafanya juhudi za kupenya zaidi baina ya nchi za Kiislamu na kupanua wigo wa ushawishi wake wa kisiasa.
Takwimu zinaonesha kuwa, tangu kuanza machafuko na vitendo vya utumiaji mabavu vya kundi la Boko Haram nchini Nigeria hadi sasa, zaidi ya watu milioni mbili wamekuwa wakimbizi na kuomba hifadhi katika nchi jirani. Aidha watu zaidi ya elfu 13 wamepoteza maisha yao katika hujuma na jinai mbalimbali zinazofanywa na Boko Haram tangu mwaka 2010 hadi sasa. Wengi wa watu hao wamepoteza maisha katika mwaka mmoja uliopita. Kwa msingi huo inaonekana kuwa, kuna mikono iliyoko nyuma ya pazia ambayo sio tu kwamba, haitaki kuona kundi la Boko Haram linatokomezwa, bali zinaona kwamba, kuimarika makundi hayo ni kwa maslahi yao.