Wanigeria waandamana kutaka Sheikh Zakzaky aachiwe huru
Waislamu wa Nigeria wamendamana katika mji wa Kaduna ulioko kaskazini mwa nchi hiyo wakitaka kuachiwa huru mara moja kiongozi wa Harakati ya Kiislamu, Sheikh Ibrahim Zakzaky anayeshikiliwa kwa miezi kadhaa sasa katika korokoro za nchi hiyo.
Maandamano hayo yaliyowashirikisha wanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria yalihutubiwa na Sheikh Abdul Majiid Bilo ambaye ameitaka serikali ya nchi hiyo kumwachia huru Sheikh Zakzaky na Waislamu wengine wanaoshikiliwa na vyombo vya usalama. Vilevile ameitaka serikali ya Abuja kukabidhi maiti za Waislamu waliouawa na jeshi la nchi hiyo ili wazikwe kwa mujibu wa sheria za Kiislamu.
Taarifa ya Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambayo imesomwa katika maandamano hayo imesema ni jambo lisilokubalika kwa jeshi la serikali iliyokula kiapo cha kulinda maisha ya raia wake kuua mamia ya watu na kutowachukuliwa hatua wanajeshi waliotenda uhalifu huo.
Disemba mwaka jana jeshi la Nigeria lilishambulia kituo cha kidini na makazi ya kiongozi wa Waislamu wa Shia nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky katika mji wa Zaria na kuua karibu Waislamu 1000. Jeshi hilo pia lilimjeruhi kwa risasi kadhaa Sheikh Ibrahim Yaqoub Zakzaky na mke wake na kuwatia mbaroni.