Rwanda yaimarisha usalama katika kukabiliana na ugaidi tarajiwa
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i14401-rwanda_yaimarisha_usalama_katika_kukabiliana_na_ugaidi_tarajiwa
Serikali ya Rwanda imetangaza kuimarisha usalama katika maeneo tofauti ya nchi hiyo kwa lengo la kuzuia kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Sep 01, 2016 03:23 UTC
  • Rwanda yaimarisha usalama katika kukabiliana na ugaidi tarajiwa

Serikali ya Rwanda imetangaza kuimarisha usalama katika maeneo tofauti ya nchi hiyo kwa lengo la kuzuia kutokea mashambulizi ya kigaidi nchini.

Kwa mujibu wa habari, hadi sasa Rwanda haijawahi kushambuliwa na magaidi, lakini pamoja na hayo serikali ya nchi hiyo imetaka kuimarishwa sana usalama na uangalizi katika maeneo ya kijamii kwa ajili ya kuzuia hujuma za aina hiyo. Miezi iliyopita polisi ya nchi hiyo ilifanya operesheni kadhaa kwa ajili ya kujiweka tayari kukabiliana na ugaidi na washukiwa wa vitendo hivyo. Aidha imeelezwa kuwa serikali ya Kigaidi hivi sasa inafanya juhudi kubwa kwa ajili ya kuzuia kuundwa mitandao ya kigaidi na kuwavutia vijana kujiunga na mitandao hiyo.

Francis Kaboneka, Waziri wa Masuala ya Serikali za Kieneo nchini Rwanda

Kwa upande wake Francis Kaboneka, Waziri wa Masuala ya Serikali za Kieneo nchini humo amewataka wakuu wa mikoa kuchukua tahadhari kubwa katika kufuatilia kuingia watu wenye misimamo mikali na makundi ya waasi kutoka nchi tofauti za Kiafrika, lengo kuu likiwa ni kuwalinda raia. Mataifa ya Libya, Nigeria, Mali, Cameroon, Chad, Somalia na Kenya ni nchi za Kiafrika ambazo zinakabiliwa na changamoto ya magenge ya kigaidi, huku mataifa ya Sudan, Sudan Kusini, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Burundi na Jamhuri ya Afrika ya Kati zikikabiliwa na changamoto zinazotokana na makundi ya waasi.