Wagabon wanaoishi Ufaransa waandamana kupinga matokeo ya uchaguzi
Raia wa Gabon wanaoishi nchini Ufaransa wameandamana kupinga matokeo ya uchaguzi wa Rais nchini kwao yaliyomrejesha tena madarakani Rais Ali Bongo.
Waandamanaji hao waliokuwa wamebeba mabango na maberamu walipiga nara za kulaani kile walichokitaja kuwa wizi wa kura uliomrejesha madarakani Ali Bongo na kusisitiza kwamba, uchaguzi huo haukuwa halali.
Waandamanaji hao wametaka mgombea wa upinzani Jean Ping atangazwe kuwa ndiye mshindi wa kiti cha urais.
Wakati huo huo, habari kutoka Libreville mji mkuu wa Gabon zinasema kuwa, hali ni shwari tangu matokeo ya uchaguzi huo yalipotangazwa na kwamba, vyombo vya usalama vimeendelea kukabiliana na waandamanaji huku watu zaidi ya elfu moja wakiwa wametiwa mbaroni.
Aidha watu watatu wameripotiwa kuuawa katika maandamano ya wapinzani mjini Libreville.
Rais Ali Bongo ambaye ndiye aliyetangazwa mshindi katika uchaguzi huo amewalalamikia wafuasi wa upinzani ambao walimiminika mitaani siku ya Jumatano na kuchoma moto bunge la nchi hiyo. Amesema demokrasia haiwezi kupatikana kwa njia kama hizo.
Siku ya Jumanne, Tume ya Uchaguzi ya Gabon ilitangaza kuwa, Rais Bongo ameshinda kiti cha urais
kwa asilimia 49.80 akifuatiwa kwa karibu na mpinzani wake mkuu Jean Ping aliyewahi kuwa Mkuu wa Kamisheni ya Umoja wa Afrika kutoka mwaka 2008 hadi 2012 ambaye amepata asilimia 48.23 ya kura. Hata hivyo wapinzani wameyakataa matokeo hayo wakisema, mgombea wao wa muungano wa upinzani Jean Ping ameporwa ushindi.
Jumuiya mbalimbali zimetoa miito ya kuchukuliwa hatua za kuzuia Gabon isije ikatumbukia katika mgogoro wa kisiasa.