Ping ataka kufanyike uchunguzi wa kimataifa kuhusu machafuko ya uchaguzi Gabon
Jean Ping mgombea wa kiti cha Urais nchini Gabon aliyeshindwa na Rais Ali Bongo katika uchaguzi wa mwezi uliopita ametoa Mwito wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana machafuko yaliyotokea baada ya kutangazwa matokeo ya uchaguzi huo.
Jean Ping amesema kuwa, kuna haja ya kufanyika uchunguzi wa kimataifa kuhusiana na ghasia zilizotokea baada ya Tume ya Uchaguzi kumtangaza Rais Ali Bongo kuwa mshindi wa kiti cha urais.
Jean Ping ametoa mwito huo wa kufanyika uchunguzi wa kimataifa katika hali ambayo, inaeelezwa kuwa kwa uchache watu sita wameuawa katika mji mkuu Libreville katika ghasia baina ya waandamanaji na vikosi vya usalama vya nchi hiyo.
Vikosi vya usalama vinatuhumiwa kwamba, vilikandamiza maandamano ya wapinzani ya kulalamikia matokeo ya uchaguzi huo na kuwafyatulia risasi wafuasi wa mrengo wa upinzani.
Wakati huo huo, safari ya ujumbe wa Umoja wa Afrika AU nchini Gabon kwa ajili ya kuutafitia ufumbuzi mgogoro wa uchaguzi imeakhirishwa. Ujumbe huo wa Umoja wa Afrika ukiongozwa na Rais Idris Deby wa Chad ambaye pia ndiye Mwenyekiti wa hivi sasa wa AU ulitarajiwa kuwasili nchini Gabon Ijumaa ya jana katika juhudi za kujaribu kuutafutia ufumbuzi mgogoro wa nchi hiyo.
Haijaelezwa ni lini tena ujumbe huo utaelekea nchini Gabon.
Matokeo ya uchaguzi huo yaliyolalamikiwa ndani na nje ya Gabon yalionyesha kwamba, Rais wa Gabon Ali Bongo ameshinda kwa kupata asilimia 49.85 huku mpinzani wake mkuu Jean Ping akipata asilimia 48.23 ya kura.