Mamia ya wahajiri haramu waokolewa katika fukwe za Libya
Maafisa wa gadi ya ulinzi wa fukwe za Italia wametangaza habari ya kuokolewa amia ya wahajiri haramu katika fukwe za Libya.
Maafisa wa gadi ya kulinda fukwe za Italia walisema jana kuwa, katika operesheni iliyofanyika jana alfajiri kwenye bahari ya Mediterranean, gadi hiyo ilifanikiwa kuwaokoa wahajiri 650 waliokuwa wamejazana kwenye boti sita zilizokuwa zimepakia watu kupindukia na ambazo zilikuwa zikirushwa na mawimbi huko na huko katika fukwe za Libya.
Kwa mujibu wa ripoti hiyo, opereshenei ya pamoja iliyofanywa na gadi ya ulinzi wa fukweni ya Italia na meli ya kikosi cha majini cha Ireland, imefanikiwa kuokoa mamia ya wahajiri hao haramu pamoja na kuopoa viwiliwili vya watu watano waliokufa maji kwenye tukio hilo.
Takwimu za hivi karibuni kabisa zilizotolewa na Shirika la Uhamiaji la Kimataifa IOM zinaonesha kuwa, tangu mwanzoni mwa mwaka huu wa 2016 hadi hivi sasa, karibu wahajiri laki moja na tano wameingia katika fukwe za Italia na wengi wao wametokea katika fukwe za Libya.
Wahajiri 726 wameripotiwa kufa maji kabla ya kufika wanakokwenda, tangu mwanzoni mwa mwaka huu hadi hivi sasa.
Tangu ulipopinduliwa utawala wa Kanali Muammar Gaddafi tarehe 20 Okroba 2012 hadi hivi sasa, Libya imezama kwenye dimbwi la mapigano ya ndani na jambo hilo limetoa fursa kwa magenge ya kigaidi na kanali za magendo ya binadamu kuelekea barani Ulaya kufanya vitendo vyao kwa uhuru nchini humo.