Mashambulizi pacha ya bomu yaua 19 Cameroon
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1552-mashambulizi_pacha_ya_bomu_yaua_19_cameroon
Kwa akali watu 19 wameuawa katika mashambulizi pacha ya bomu yaliyolenga soko moja katika mji wa Meme, kaskazini mwa Cameroon.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 19, 2016 10:15 UTC
  • Mashambulizi pacha ya bomu yaua 19 Cameroon

Kwa akali watu 19 wameuawa katika mashambulizi pacha ya bomu yaliyolenga soko moja katika mji wa Meme, kaskazini mwa Cameroon.

Duru za kijeshi nchini humo zimeripoti kuwa, washambuliaji wawili wa kujitolea muhanga waliokuwa wamevaa mafulana yenye mada za milipuko wamelishambulia soko hilo mapema leo na kusababisha vifo vya watu 19 na wengine zaidi ya 50 kujeruhiwa. Hadi tunaenda mitamboni, hakuna kundi lolote lililokuwa limekiri kuhusu na hujuma hiyo ya leo Ijumaa ingawa kundi la kigaidi na kitakfiri la Boko Haram limekuwa likitekeleza mashambulizi ya aina hii nchini humo kila uchao. Mwishoni mwa mwezi uliopita wa Januari, watu 25 waliuawa baada ya kutokea mashambulio manne ya wanamgambo waliojiripua kwa mabomu, katika kijiji cha Bodo kaskazini mwa Cameroon. Zaidi ya watu 1,200 wameuawa katika hujuma za Boko Haram nchini Cameroon tangu lililopoanzisha mashambulizi yake dhidi ya nchi hiyo mwaka 2013.

Kundi la Boko Haram limepanua mashambulizi yake kutoka Nigeria hadi katika nchi jirani za Chad, Cameroon na Niger. Inadaiwa kuwa kuna wanamgambo 8700 wa Boko Haram kwenye eneo hilo.