Museveni ashinda urais Uganda, upinzani wakataa matokeo
Tume ya uchaguzi ya Uganda imemtangaza Yoweri Kaguta Museveni kuwa mshindi wa kiti cha rais kwenye uchaguzi mkuu uliofanyika siku ya Alhamisi.
Mwenyekiti wa Tume hiyo, Badru Kiggundu amesema Museveni amejipatia takriban asilimia 62 ya kura zote zilizopigwa huku mpinzani wake wa karibu, Kizza Besigye akishika nafasi ya pili kwa kujipatia asilimia takriban asilimia 34 ya kura zote. Museveni aligombea kwa tiketi ya chama cha NRM, naye Besigye akawania kwa tiketi ya FDC. Mgombea binafsi na Waziri Mkuu wa zamani, Patrick Amama Mbabazi ameibuka wa tatu kwa kujipatia takriban asilimia 2.
Huku hayo yakijiri, chama cha FDC kimesema hakitambui matokeo ya uchaguzi na kudai kwamba chama tawala kimetumia hila na udanganyifu ili kupata ushindi. Mkuu wa chama hicho, Mugisha Muntu ameitaka jamii ya kimataifa kukatalia mbali matokeo hayo na kuwawajibisha waliohusika na kile alichotaja kuwa ni wizi wa kura. Muntu amesema kukamatwa mgombea urais wa FDC wakati zoezi la kuhesabu kura likiendelea, kunaonyesha wazi kwamba serikali ilikuwa na jambo la kuficha. Hii ni mara ya nne kwa daktari Kizza Besigye kugombea urais na kushindwa nchini Uganda.