Sep 28, 2016 02:39 UTC
  • Muwahhabi aliyebomoa turathi za Kiislamu Mali afungwa miaka tisa jela

Muwahhabi mwenye misimamo mikali, Ahmed Al-Faqi Al-Mahdi amepatikana na hatia ya uhalifu wa kivita na kuhukumiwa miaka 9 jela katika Mahakama ya Kimataifa ya Jinai ICC.

Mahakama hiyo imesema Al-Mahdi alihusika katika uharibifu wa makusudi wa turathi za Kiislamu nchini Mali ambapo alihujumu makavazi tisa na lango la siri la Msikiti wa Sidi Yahia mwaka 2012.

Maeneo hayo yaliyo katika mji wa kale wa Timbuktu Mali yako katika orodha ya Turathi za Dunia ya Shirika la Umoja wa Mataifa la Elimu Sayansi na Utamaduni UNESCO.

Jaji Raul Cano Pangalangan aliyesoma hukumu ya Al-Mahdi amesema, "Mahakama kwa kauli moja inakuhukumu k miaka tisa jela. Kwa mujibu wa kanuni za rufaa, muda uliokuwepo rumande tangu ukamatwe tarehe 18 Septemba mwaka 2015 utapunguzwa kwenye hukumu yako."

Akizungumzia hukumu hiyo mkurugenzi mkuu wa UNESCO Irina Bokova amesema ni ya kihistoria katika kutambuliwa kwa umuhimu wa urithi kwa ubinadamu kwa ujumla na wanajamii ambazo zimeuhiifadhi kwa karne kadhaa.

Magaidi wa Kiwahhabi wakiharibu turathi za Kiislamu Mali

Pia inasaidia dhamira ya UNESCO kwamba urithi una jukumu kubwa katika ujenzi wa amani, na ameongeza kuwa uamuzi huo ambao ni wa kwanza chini ya mkataba Roma, ni hatua muhimu sana katika kumaliza ukwepaji sheria katika masuala ya uharibifu wa urithi wa kiutamaduni.

Waasi wa kundi la Kiwahabbi linalojiita Ansaruddin huko kaskazini mwa Mali waliharibu idadi kubwa ya turathi za Kiislamu Mali mwaka 2012 ikiwa ni pamoja na kubomoa makaburi ya Mawalii wa Mwenyezi Mungu.

Aghalabu ya wakaazi wa kaskazini mwa Mali na hasa Timbuktu ni Masufi au watu wa Twariqa ambao hufanya ziara katika makaburi ya Mawalii mara kwa mara. Kundi la Ansaruddin linalofuata itikadi za kufurutu ada za Kiwahhabi linapinga mila na desturi hiyo ya Kiislamu.

 

Tags