Shaka ya waangalizi wa Ulaya kuhusu usahihi wa uchaguzi wa Uganda
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i1648-shaka_ya_waangalizi_wa_ulaya_kuhusu_usahihi_wa_uchaguzi_wa_uganda
Waangalizi wa Ulaya wamesema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikuwa huru katika uchaguzi wa hivi karibuni.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Feb 21, 2016 04:30 UTC
  • Shaka ya waangalizi wa Ulaya kuhusu usahihi wa uchaguzi wa Uganda

Waangalizi wa Ulaya wamesema kuwa Tume ya Uchaguzi ya Uganda haikuwa huru katika uchaguzi wa hivi karibuni.

Edward Kukan mkuu wa timu ya uangalizi ya Umoja wa Ulaya katika uchaguzi mkuu wa hivi karibuni nchini Uganda amesema kuwa chama tawala cha Rais Yoweri Museveni, National Resistance Movement, kiliharibu mazingira ya uchaguzi wa hivi karibuni nchini humo, kwa kuzua hofu na wasiwasi dhidi ya viongozi wa upinzani na wafuasi wao. Siku ya kufanyika uchaguzi huo mkuu hapo Alhamisi iliyopita, vituo vingi vya kupigia kura na hasa katika mji mkuu, Kampala, vilifunguliwa kwa kuchelewa. Hali kadhalika polisi na askari usalama walivamia na kuwapiga wapigaji kura katika maeneo kadhaa mjini Kampala. Kizza Besigye mpinzani mkuu wa Rais Yoweri Museveni na ambaye alipata nafasi ya pili katika uchaguzi huo siku ya Ijumaa alikamatwa na askari usalama kwa mara ya tatu katika kipindi cha juma moja na kuachiliwa huru masaa kadhaa baadaye. Hata hivyo nyumba yake bado imezingirwa na polisi. Polisi inawatuhumu wapinzani kuwa wanapanga kutangaza matokeo tofauti ya uchaguzi kinyume na yale yaliyotangazwa rasmi na tume ya uchaguzi. Tume hiyo ya uchaguzi imemtangaza Rais Yoweri Museveni ambaye ameingoza nchi hiyo kwa miongo mitatu sasa kuwa mshindi wa uchaguzi huo kwa kupata zaidi ya asilimia 60 ya kura.