Askari wa Niger na Chad waua wanachama 123 wa Boko Haram
Operesheni ya pamoja ya kijeshi ya Niger na Chad imepelekea kuuawa wanamgambo 123 wa kundi la Boko Haram.
Wizara ya Ulinzi ya Niger imetangaza kuwa, wanachama 123 wa kundi la kigaidi la Boko Haram wameuwa na kikosi cha pamoja cha nchi hiyo na Chad tangu Julai mwaka huu.
Kanali Mustapha Ledru, msemaji wa Wizara ya Ulinzi ya Niger amesema kuwa, mamia ya wanachama wa kundi hilo pia wamejeruhiwa huku kikosi hicho cha pamoja dhidi ya Boko Haram kikifanikiwa kukamata idadi kubwa ya silaha na za za kivita.
Kundi la kigaidi la Boko Haram lenye makao yake kaskazini mashariki mwa Nigeria limepanua wigo wa harakati zake katika miaka ya hivi karibuni hadi katika nchi jirani za Cameroon, Niger na Chad.
Hatua hiyo ilepelekea nchi hizo kuunda kikosi cha pamoja cha kukabiliana na wanamgambo hao wa Boko Haram na kwa mujibu wa maafisa wa kijeshi wa nchi hizo, operesheni hiyo ya pamoja dhidi ya wangambo hao imekuwa na mafanikio.
Watu wasiopungua 20 elfu wameripotiwa kuuawa na wengine milioni mbili na laki sita wamepoteza makazi yao tangu kundi hilo la kitakfiri lilipoanzisha mashambulizi yake nchini Nigeria mwaka 2009.
Aidha mashambulio hayo ya Boko Haram yamevuruga maisha ya kawaida ya wananchi wa kaskazini mashariki mwa Nigeria na katika maeneo ya mpakani mwa nchi hiyo ya magharibi mwa Afrika.