Sudan: Madai kwamba tulitumia silaha za kemikali Darfur, hayana ukweli
Serikali ya Sudan imekadhibisha madai ya Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International lililodai kwamba Khartoum ilitumia silaha za kemikali katika jimbo la Darfur.
Taarifa iliyotolewa na serikali ya Sudan imeitaja ripoti hiyo kuwa ya uongo na isiyo na ukweli wowote ule. Muhammad Hamid, naibu mkuu wa chama cha Kongresi ya Kitaifa nchini Sudan amesema kuwa, lengo la kutolewa madai hayo ni kutaka kudhoofisha serikali ya Khartoum. Ameongeza kuwa, hata tuhuma za ukiukaji wa haki za binaadamu zilizotolewa kipindi cha nyuma dhidi ya serikali ya Sudan, zilitekelezwa kwa msingi huo.

Wiki iliyopita, Shirika la Msamaha Duniani la Amnesty International lilitoa ripoti likiituhumu serikali ya Sudan kwamba ilitumia silaha hatari za kemikali dhidi ya raia wakiwemo watoto wadogo miezi minane iliyopita. Katika upande miwingine, duru mpya ya mazungumzo ya kitaifa nchini Sudan imepangwa kufanyika tarehe 10 mwezi huu wa Oktoba mjini Khartoum. Mtakumbuka kuwa, eneo la Darfur limekuwa likishuhudia machafuko kwa kipindi cha miaka 13 sasa.