Harakati ya Kiislamu yapigwa marufuku Kaduna, Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i16969-harakati_ya_kiislamu_yapigwa_marufuku_kaduna_nigeria
Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky imepigwa marufuku katika jimbo la Kaduna huku Waislamu wakiendelea kukandamizwa nchini humo.
(last modified 2026-02-05T09:20:29+00:00 )
Oct 08, 2016 03:18 UTC
  • Harakati ya Kiislamu yapigwa marufuku Kaduna, Nigeria

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria inayoongozwa na Sheikh Ibrahim Zakzaky imepigwa marufuku katika jimbo la Kaduna huku Waislamu wakiendelea kukandamizwa nchini humo.

Katika taarifa siku ya Ijumaa, serikali ya Jimbo la Kaduna imeonya kuwa, yeyeote atakayepatikana kuwa mwanachama wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria atafungwa jela miaka saba au atatozwa faini au yote mawili kwa pamoja.

Aidha serikali ya Kaduna imedai kuwa, Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ambayo aghalabu ya wanachama wake ni Waislamu wa madhehebu ya Shia wanashiriki katika maandamano yasiyo na kibali na kuzuia magari barabarani tangu Desemba mwaka jana.

Ikumbukwe kuwa kati ya Desemba 12-14 mwaka 2015, Jeshi la Nigeria liliwashambulia wafuasi wa Harakati ya Kiislamu Nigeria IMN katika mji wa Zaria jimboni Kaduna kaskazini mashariki mwa nchi hiyo. Jeshi lilidai kuwa wafuasi wa IMN walikuwa na njama ya kutaka kumuua Mkuu wa Jeshi la Nigeria, madai ambayo yamekanushwa vikali na wafuasi wa harakati hiyo. Jeshi hilo katili liliizika miili ya waliouawa katika kaburi moja kwa lengo la kuficha ushahidi wa ukubwa wa jinai hiyo.

Ukatili wa jeshi la Nigeria dhidi ya Waislamu

Harakati ya Kiislamu ya Nigeria hata hivyo inasisitiza kuwa zaidi ya Waislamu 1000 waliuliwa na jeshi la nchi hiyo katika hujuma hiyo.

Aidha Jeshi la Nigeria lilimkamata Sheikh Ibrahim Zakzaky, Kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya Nigeria akiwa pamoja na mke wake. Hali ya kiafya ya Sheikh Zakzaky inaripotiwa kuwa mbaya huku taarifa zikisema amepoteza jicho moja mbali na kuwa na majeraha mengine mwilini. Serikali ya Nigeria inamshikilia kiongozi huyo wa Kiislamu tokea Desemba mwaka jana pasina kumfungulia mashtaka.