Obasanjo ataka upinzani na serikali kuzungumza Uganda
Serikali na upinzani nchini Uganda zimetakiwa kukomesha uhasama wa kisiasa na badala yake zikae kwenye meza ya mazungumzo na kutatua hitilafu zilizoko kwa amani.
Rais wa zamani wa Nigeria, Olusegun Obasanjo, ameitaka serikali ya Uganda kuketi kwenye meza ya mazungumzo na pinzani ili kuondoa wingu la uhasama lililotanda kufuatia uchaguzi mkuu uliomalizika siku chache zilizopita.
Obasanjo ambaye aliongoza ujumbe wa Jumuiya ya Madola uliokuwa ukiangalia vigezo vya kidemokrasia katika uchaguzi uliokamilika nchini Uganda, amewashauri viongozi wa uganda kujiepusha na makabiliano na migongano baina yao. Rais wa zamani wa Nigeria amekemea jinsi serikali inavyotumia mkono wa chuma kuwadhibiti wapinzani na kutaka uhuru wa kujieleza uheshimiwe. ''Dosari zilizoshuhudiwa katika uchanguzi mkuu zimeathiri matokeo na kutilia shaka ukweli, haki na uwazi wa uchaguzi huo'' amesema kiongozi huyo wa zamani wa Nigeria. Hata hivyo amesisitiza kuwa, tofauti kati ya serikali na upinzani zinahitajika kusuluhiswa kupitia mazugumzo.''