Wapinzani Nigeria wataka marekebisho ya Katiba
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17506-wapinzani_nigeria_wataka_marekebisho_ya_katiba
Vyama vya upinzani nchini Nigeria vimetaka kufanyike mabadiliko ya sheria za chaguzi za miji katika katiba ya nchi hiyo.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 15, 2016 23:09 UTC
  • Wapinzani Nigeria wataka marekebisho ya Katiba

Vyama vya upinzani nchini Nigeria vimetaka kufanyike mabadiliko ya sheria za chaguzi za miji katika katiba ya nchi hiyo.

Muungano wa vyama 16 vya upinzani umetoa tamko la pamoja na kulitaka bunge la nchi hiyo lifanyie marekebisho katiba ya nchi hiyo ili kuruhusu tume huru ya uchaguzi ya Nigeria kusimamia chaguzi za mabaraza ya miji.

Muungano huo wa vyama vya kisiasa umesema kuwa, hauna imani na tawala za kieneo nchini Nigeria kwani zina historia ya kufanya udanganyifu katika chaguzi za majimbo kwa manufaa ya chama tawala.

Ramadnai ya jimbo la Ogun nchini Nigeria

 

Vyama hivyo vimetoa ushahidi katika uchaguzi wa tarehe 8 Oktoba wa serikali za mitaa nchini Nigeria na kuongeza kuwa, kulifanyika udanganyifu mkubwa katika jimbo la Ogun la kusini magharibi mwa Nigeria na kuwapa ushindi wagombea wote wa chama cha Rais Muhammadu Buhari.

Tamko la muungano wa vyama vya upinzani nchini Nigeria limeongeza kuwa, serikali za kieneo katika jimbo la ogon lilitumia vitisho na kuwatia khofu wapiga kura sambamba na kuchakachua matokeo ya uchaguzi huo wa Oktoba 8.