IHRC: Saudia inashiriki kukandamiza Harakati ya Kiislamu Nigeria
https://parstoday.ir/sw/news/africa-i17827-ihrc_saudia_inashiriki_kukandamiza_harakati_ya_kiislamu_nigeria
Kamisheni ya Haki za Binadamu za Kiislamu (IHRC) yenye makao yake mjini London Uingereza imetangaza kuwa, nyaraka zilizofichuliwa na mtandao wa WikiLeaks zinathibitisha kwamba Saudi Arabia inashiriki katika kukandamiza Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria.
(last modified 2023-11-27T08:44:11+00:00 )
Oct 20, 2016 23:53 UTC
  • IHRC: Saudia inashiriki kukandamiza Harakati ya Kiislamu Nigeria

Kamisheni ya Haki za Binadamu za Kiislamu (IHRC) yenye makao yake mjini London Uingereza imetangaza kuwa, nyaraka zilizofichuliwa na mtandao wa WikiLeaks zinathibitisha kwamba Saudi Arabia inashiriki katika kukandamiza Harakati ya Kiislamu nchini Nigeria.

Mwenyekiti wa kamisheni hiyo, Massoud Shadjareh amesema kuwa, nyaraka zilizofichuliwa na WikiLeaks zinaonesha kuwa, Saudia ina nafasi kubwa katika kuwakandamiza wanachama wa Harakati ya Kiislamu inayoongowa na Sheikh Ibrahim Zakzaky nchini Nigeria. Akizungumzia jinsi serikali ya Nigeria ilivyopiga marufuku shughuli za maombolezo na kukumbuka mauaji ya mjukuu wa Mtume Muhammad (saw), Imam Hussein (as) nchini Nigeria, Massoud Shadjareh amesema: Harakati ya Kiislamu ya Nigeria ni jumuiya ya amani inayotoa changamoto kwa dhulma na ufisadi katika taasisi za serikali ya Abuja. Amesema inaonekana kuwa serikali ya sasa ya Nigeria inaunga mkono viongozi wabadhirifu na kwa sababu hiyo inapinga shughuli za Harakati ya Kiislamu ya nchi hiyo.

Mwenyekiti wa Kamisheni ya Haki za Binadamu za Kiislamu amesema serikali ya Nigeria inaitambua Harakati ya Kiislamu kuwa ni kikwazo kutokana na kuwa na wafuasi karibu milioni 15 kote nchini na kwa msingi huo inaiogopa taasisi hiyo ya kiraia.

Sheukh Zakzaky

Tarehe 13 Desemba mwaka jana jeshi la Nigeria liliua mamia ya Waislamu katika shambulio dhidi ya kituo cha kidini cha Husainiyyah ya Baqiyyatullah katika mji wa Zaria. Katika shambulio hilo, jeshi hilo lilimjeruhi vibaya, kumkamata kiongozi wa Harakati ya Kiislamu ya nchini humo Sheikh Ibrahim Zakzaky pamoja na mkewe baada ya kuua watoto wake kadhaa.